
JINA la kiungo mshambuliaji wa TP Mazembe, Owe Bonganya, linajadiliwa kwenye mipango ya usajili ya Yanga kwenye dirisha hili dogo linalotarajiwa kufungwa keshokutwa Jumatano huku taarifa zikiwepo za kusitisha mipango ya kumsajili.
Kiungo huyo alitua nchini wiki iliyopita kwa ajili ya kufanya majaribio katika timu hiyo ambayo hadi sasa imefanya usajili mzito wa wachezaji watano.
Wachezaji hao waliosajiliwa na Yanga ni kiungo fundi Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Yikpe Gnamien, Adeyum Saleh, Ditram Nchimbi na Tariq Seif ambao tayari wamejiunga na kikosi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, kiungo huyo ameshindwa kuwashawishi viongozi wa benchi hilo baada ya kushindwa kuonyesha kiwango kizuri kwa muda wa wiki moja aliofanya mazoezi na Yanga.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo ana kiwango cha kawaida tofauti na walivyotarajia baada ya kushindwa kuonyesha umahiri wake wa kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao.
Aliongeza kuwa, kiungo huyo amezidiwa uwezo na kiungo mshambuliaji Mzambia, Eric Kabamba aliyekuwa anakipiga Buildcon ya nchini kwao kabla ya kufuzu majaribio hayo huku akisubiria mkataba wa miaka miwili Yanga.
“Upo uwezekano mdogo wa Bonganya kusajiliwa Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo unaoendelea baada ya kushindwa kuwashawishi viongozi wa benchi la ufundi.
“Bonganya alipewa muda wa wiki moja kufanya majaribio kabla ya kupewa mkataba wa miaka miwili ambapo ameshindwa kuwaonyesha uwezo.
“Hivyo nafasi yake huenda ikachukuliwa na Eric raia wa Zambia aliyekuwa anaichezea Builcon ambaye ameonyesha kiwango kikubwa cha kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Hersi Said, anayewezesha kutoa fedha katika usajili wa Yanga, alisema: “Huyo mchezaji tulimleta kwa ajili ya kufanya majaribio na siyo kusajiliwa kwa lengo la kuangalia uwezo wake kabla ya kumsajili, hivyo kama benchi la ufundi limeona hana uwezo, basi tutaachana naye.”
Wilbert Molandi, Dar es Salaam