
NDOA ni jambo la furaha na sifa katika jamii nyingi mbali na kuwa miongoni mwa vitu vinavy-owapa wahusika heshima katika jamii.
Kwa tamaduni za Kiafrika, mara nyingi wanaume ndio hubeba jukumu la kuwa waamuzi wa suala hilo.
Japo jambo hilo ni la kheri, wapo mastaa wa kiume Bongo ambao kwa namna moja au nyingine wamelipa kisogo suala hilo.
Leo nimekusogezea orodha ya wasanii wa Bongo Fleva ambao licha ya kuwa wakongwe, wameamua kuendelea kuwa mabachela (mabachela wa muda wote):
- MADEE
Hakuna asiyefahamu juu ya ukongwe wa msanii huyu katika tasnia ya Bongo Fleva, ni miongoni mwa wasanii wachache wa kitambo ambao bado wapo kwenye ramani.
Msanii huyo ambaye alijipatia umaarufu miaka ya 2000 akiwa miongoni mwa wasanii waliounda Kundi la Tip Top Connection, licha ya kuwa katika mahusiano mara kadhaa na kubahatika kupata watoto watatu, lakini hajabahatika kufunga ndoa. Hivyo, anaendelea kuwa miongoni mwa wasanii mabachela nguli.
- JOH MAKINI
John Saimon ‘Joh Makini’ ni miongoni mwa wasanii wakongwe sana kunako gemu ya Bongo Fleva hasa katika kipengele cha muziki wa kufoka yaani Hip Hop.
Alianza kutambulika akiwa katika kundi la Nako 2 Nako miaka ya 2000. Licha ya kupata mafanikio makubwa katika muziki huo ikiwa ni pamoja na kudumu kwenye fani kwa muda mrefu lakini ameshindwa kufurukuta linapokuja suala la kufunga ndoa na anakuwa miongoni mwa wasanii wanaounda orodha hii ya wasanii waliozipa kisogo ndoa.
- T.I.D
Khalid Mohamed almaarufu kama T.I.D, alianza kupata umaarufu miaka ya 2000 baada ya kuachia ngoma yake ya Zeze ambayo ilikuwa gumzo na nyimbo pendwa kwa wakati huo. Aliendelea kufanya poa kwa nyimbo mbalimbali kama Nyota Yako, Kiuno, Siamini na nyingine nyingi.
Kiufupi jamaa ni ‘don town’ kitambo na umri ni mkubwa kinoma lakini suala la kuvuta jiko limegonga mwamba, bado yupo yupo sana ambapo licha ya kutooa lakini pia inasemekana jamaa bado anaishi kwao.
- DUDU BAYA
Huyu pia ni miongoni mwa wasanii wa kitambo sana kwani alianza gemu mwishoni mwa miaka ya tisini na kupata umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 2000. Miongoni mwa nyimbo zilizompa umaarufu ni pamoja na Umeondoka, Nakupenda Tu, Nakupenda Mpenzi na nyingine kibao. Kiufupi jamaa umri unamtupa mkono licha ya kubahatika kupata watoto kadhaa lakini jamaa bado hajavuta jiko.
- Q – CHILLAH
Ni mmoja kati ya malejendari wa Bongo Fleva, amefanya makubwa sana kwenye muziki huo. Miongoni mwa ngoma zake za kitambo ni pamoja na My Boo, Si Ulinikataa, Uhaligani na nyingine kibao. Ameonesha ukomavu mpaka kwa vijana wa sasa kama kina Harmonize kwa kufanya nao kolabo lakini suala la kufunga ndoa bado ni mtihani licha ya kuwa na watoto.
- KING CRAZY GK
Huyu alikuwa kiongozi wa Kundi lililowahi kusumbua kinoma miaka ya 2000 lililokwenda kwa jina la East Coast Team. Wapinzani wao wakubwa walikuwa ni TMK Wanaume Family chini ya kiongozi wao Juma Kassim ‘Nature’. Katika kundi lao, Gwamaka Kaihula ‘GK’ alikuwa na wenzake wakiwemo Ambwene Yesaya ‘AY’ na Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ ambao wote wameshavuta majiko lakini mwamba huyu bado anaendelea ‘kula kwa mama ntilie’.
GK alitamba na ngoma kali kama Sauti ya Manka na Nitakufaje. Kundi lao lilisambaratika na sasa kila mmoja anatoa ngoma kimpango wake. AY na FA wameendelea kuwa kwenye mainstream lakini GK amekuwa kimya sana.