×

Zidane Aanza Kuyakusanya Tena

KOCHA wa Real Madrid, Zinedine Zidane ameendelea kuonyesha umwamba wake kwenye soka baada ya kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Super Cup.

 

Madrid walikuwa wanavaana na wapinzani wao wakubwa Atletico Madrid, ambapo walifanikiwa kumaliza dakika 120 kwa suluhu lakini wakaibuka na ushindi wa penalti 4-1.

Hili ni kombe la kwanza la kocha huyo msimu huu na bado ana kazi kubwa sana ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Hispania, La Liga, baada ya kuwa na kasi nzuri.

 

Mechi hii ilikuwa ikionyesha upinzani wa hali ya juu na kuonyesha ule umahiri wa Atletico na Madrid.

Kulikuwa na vita kubwa sana kati ya mastaa wa timu hizo, Alvaro Morata kutoka Atletico na Sergio Ramos kutoka Real Madrid.

 

Hata hivyo, dakika za nyongeza Federico Valverde wa Real alipewa kadi nyekundu lakini bado haikuwa na msaada kwa Atletico Madrid.

Real Madrid wanatakiwa kumshukuru sana kipa wao Thibaut Courtois, ambaye alifanya kazi kubwa sana wakati wa mikwaju ya penalti kwenye mchezo huo uliopigwa nchini Saudia Arabia.

 

Upinzani wa Madrid na Atletico kwenye La Liga ni wa hali ya juu kwa kuwa ni majirani na viwanja vyao vipo umbali wa mita 10 tu.

Hata hivyo, wachambuzi wa ligi hii wamekuwa wakisema kuwa mara kwa mara anayeshinda ubingwa huu huwa yule ambaye ametwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita lakini kwa msimu huu hakuna hata mmoja.

 

Awali kwenye mchezo huo tiketi ziliuzwa zote 62,000, lakini baada ya Barcelona kutolewa kwenye nusu fainali ya Atletico mashabiki waliokuwa wakitaka kumuona Lionel Messi waligoma kuingia uwanjani na watu 59,000 tu, ndiyo waliingia kutazama mechi hiyo.

Sergio Ramos, ambaye ni nahodha aliyefanikiwa zaidi kwa kizazi hiki alionyesha kiwango cha juu sana kwenye mchezo huo ambapo aliifungia timu yake mkwaju muhimu.

Mara baada ya mchezo huo, alisema kuwa walikuwa wanaamini kuwa watakutana na upinzani kwa Atletico kwa kuwa ni moja ya timu bora Hispania.

“Haina shaka sana kwa hili tulilokutana nalo, tulijiandaa kwa mapambano na kila mmoja alifahamu kuwa Atletico siyo timu ndogo.

 

“Kila mmoja alikuja hapa akiwa anafahamu kuwa tunakwenda kucheza mchezo mgumu na matokeo haya ni mazuri kwetu kwa kuwa tumeanza msimu vizuri.

“Hili ni kombe la kwanza, lakini naamini kuwa bado tunaweza kuchukua Ligi Kuu Hispania na Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kombe lingine kwa kuwa tuna kikosi imara,” alisema Ramos ambaye ametwaa ubingwa huu mara nne.

 

Haya yanaonekana kuwa mafanikio makubwa tena kwa Zidane kwenye kikosi cha Real Madrid likiwa ni kombe lake la tatu la Super Cup.

Madrid wanashika nafasi ya pili kwa timu zilizotwaa ubingwa huu mara nyingi, ikiwa imeutwaa mara 11, mara mbili nyuma ya Barcelona ambao wametwaa mara 13.

 

Zidane anaonekana kufanikiwa kuliko makocha wote kwenye ligi hiyo kwa sasa akiwa ameshatwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu na Klabu Bingwa Dunia ametwaa mara mbili na La Liga mara moja.

Kocha huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Madrid, aliondoka kwenye timu hiyo na kurejea tena, lakini wengi wakaamini kuwa hawezi kwenda tena na kasi ya makombe.

 

“Tunaendelea kutafuta makombe mengine, kila tukilala tunawaza kuhusu makombe, kila mchezaji hapa anafahamu kuwa mafanikio makubwa zaidi ya Real Madrid ni makombe, hivyo tunapambana kuona mwisho wetu msimu huu utakuwaje,” alisema Zidane raia wa Ufaransa.

LONDON, England

Leave a Comment