
KESHO Jumapili, Liverpool itakuwa mwenyeji wa Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England utakaochezwa kwenye Uwanja wa Anfield kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Huu ni mchezo ambao unaonekana kama utakuwa wa upande mmoja kutokana na Liverpool hivi sasa kuwa juu zaidi ya Man United.
Katika msimamo wa Ligi Kuu England, Liverpool inaongoza ikiwa na pointi 61 zilizotokana na kushinda mechi 20 na sare moja. Mpaka sasa haijapoteza hata mechi moja kati ya mechi 21 ilizocheza msimu huu.
Kiwango bora cha Liverpool msimu huu kinazifanya timu nyingi zikienda kucheza dhidi yake zinakuwa na wasiwasi mkubwa sana.
Man United ina pointi 34 katika nafasi ya tano baada ya kucheza mechi 22, yenyewe imepoteza mechi sita. Imeachwa pointi 27 na Liverpool.
Licha ya kwamba wengi wanaamini mchezo huo unaweza kuwa wa upande mmoja, lakini Man United inaweza kufanya jambo kubwa sana dhidi ya Liverpool.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Man United iliisumbua sana Liverpool na ndiyo timu pekee hadi sasa imeambulia pointi dhidi ya timu hiyo.
Marcus Rashford alianza kuifungia Man United dakika ya 36, Lioverpool ikasubiri hadi dakika ya 85 ndipo ikasawazisha bao hilo kupitia kwa Adam Lallana ambaye alitokea benchi.
Wengi hawakuamini kama Man United ingeweza kucheza vizuri kipindi hicho wakati Liverpool ikionekana moto kama ilivyo hivi sasa.
Kuelekea mchezo wa keshokutwa, takwimu zinaonyesha kwamba, timu hizo zimekutana mara 231. Man United imeshinda 88, Liverpool imeshinda 76 na sare 67.
Ukiangalia matokeo katika mechi zao tano zilizopita, kila mmoja ameshinda moja na sare tatu.
Matokeo hayo yapo hivi; Liverpool 0-0 Man United, Man United 2-1 Liverpool, Liverpool 3-1 Man United, Man United 0-0 Liverpool na Man United 1-1 Liverpool.
Jurgen Klopp ambaye ni kocha wa Liverpool, anasema: “Tunahitaji kucheza kwa kuiheshimu kila timu, hatupo tayari kuona tunashindwa kumalizia mwanzo mzuri tulioanza nao.”
Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer, anasema: “Tunakwenda kukutana na timu iliyo kwenye nafasi nzuri, lakini tutafanya kila lililo bora kupata matokeo mazuri dhidi yao.”
LIVERPOOL, England