×

Denti la Sita Abakwa Akitoka Saluni

MARA: Denti wa darasa la sita katika shule moja ya msingi iliyopo Kata ya Ring’wani Tarafa ya Ikorongo wilayani Serengeti, Mara, anadaiwa kubakwa alipokuwa akitoka saluni kunyoa.

 

Mtoto huyo wa kike ambaye jina limehifadhiwa kwa sababu za kimaadili, amelazwa katika Hospitali ya Nyerere DDH baada ya kubakwa na mtu asiyejulikana.

Tukio hilo ambalo limekuwa gumzo wilayani humo, lilijiri Januari 12, mwaka huu, muda wa saa 11 jioni wakati mtoto huyo akitoka kunyoa kwenye saluni moja iliyopo eneo la Kijuweni.

 

Akizungumza kwa taabu na Gazeti la IJUMAA akiwa wodini kwenye hospitali hiyo, mtoto huyo alisema, alikutwa na mkasa huo alipokuwa akikatiza barabarani baada ya kukutana na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Boni.

 

Alisema alipokutana na mtu huyo, alimuita, lakini hakumtilia shaka kwa kuwa anamfahamu.

Alisema kuwa, ghafla, mtu huyo alimshika mkono na kuanza kumburuza, akimvutia kichakani huku akimtisha kuwa kama atakataa, atamuua.

 

“Aliniburuza hadi kichakani huku akitishia kunichoma kisu alichokuwa nacho endapo nitapiga kelele.

“Niliogopa sana ndipo akanipiga mtama, nikaanguka kisha akanibana na Kuniingilia.

“Kiukweli niliumia sana na kuishiwa nguvu, alipomaliza kuniingilia, alijitoa huku akiendelea kutishia kuniua,” alisema mtoto huyo kwa uchungu.

 

Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto huyo aliyetajwa kwa jina moja la Shida, alisema mtoto wake alipokaribia nyumbani

aliishiwa nguvu na kujikuta akianguka kwenye shamba la mahindi hadi alipokutwa na watoto wa shemeji yake waliokuwa wanatafuta mboga.

 

Alisema baada ya watoto hao kumuona, ndipo walipomtaarifu kaka yake ambaye alikwenda kumchukua bila kujua alikuwa amepatwa na tatizo gani.

“Nguo zilikuwa zimeloa damu. Walimchukua hadi nyumbani, lakini walipomfikisha nyumbani alianguka tena na kupoteza fahamu.

 

“Kufuatia hali hiyo, nilipigiwa simu kuwa kuna tatizo nyumbani, kwa kweli nilipofika sikuwa katika hali ya kawaida.

“Baada ya mwanangu kuzinduka, nilimuuliza, akasema amebakwa na kumtaja mtuhumiwa,” alidai mama huyo.

 

Huku akizungumza kwa unyonge, mama huyo aliendelea kusema kuwa, hatua ya kwanza alikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji na Kijiji kisha alimchukua mwanaye kwa bodaboda hadi kituo kidogo cha Polisi ambapo alipewa fomu ya matibabu (PF-3) na kumkimbiza hospitalini ambako amelazwa.

 

Mganga wa zamu aliyejitambulisha kwa jina moja la Jose alisema kuwa mtoto huyo alikuwa amechanika mno sehemu yake ya siri, hivyo walilazimika kumshona na sasa anaendelea na dawa. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji; Tente Wambura alisema baada ya kupata taarifa walianza ufuatiliaji.

 

“Tumeambiwa mtuhumiwa ametoroka na huwenda huwa anarudi nyumbani usiku.

“Tumeweka mitego yetu kuhakikisha tunamkamata na kumfikisha Polisi,” alisema mwenyekiti huyo.

 

Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji; Philipo Rhobi alisema, awali walisikia mtuhumiwa alikimbilia Kijiji cha Nyamatoke. Katika ufuatiliaji ilibainika kuwa ameenda Michuri.

“Polisi walishafika hapa, tunashirikiana kumsaka, naamini tutampata tu,” alisema.

 

Polisi wilayani Serengeti walisema wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huku wakiomba wananchi wawasaidie kumfichua. Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, kwa msisitizo alisema watahakikisha wanamkamata mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

“Hata atakayebainika kumficha, tukimkuta tutamsomba kwa kushiriki kuficha mhalifu, utamaduni wa kubaka na kulawiti haukuwepo kabisa. Naona unaanza kushika kasi, dawa ni kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema DC Babu.

Stori: MWANDISHI WETU, Ijumaa

Leave a Comment