×

JIPANGE NA PEPA KUANZA KUTIMUA VUMBI MASHULENI

Programu maalum yenye lengo la kuwajengea wanafunzi wa sekondari uwezo wa kukabiliana na mitihani yao ya mwisho iitwayo Jipange na Pepa, inatarajiwa kuanza kupelekwa kwenye shule mbalimbali za sekondari, za serikali na binafsi kwa lengo la kutoa elimu kwa wanafunzi.

Katika programu hiyo inayoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Risasi, Amani na Ijumaa Wikienda, mitihani iliyotungwa kwa mfumo wa NECTA na walimu wazoefu, huchapishwa magazetini katika toleo moja huku majibu yakitolewa katika toleo linalofuatia, kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi kila wiki.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Mratibu wa Programu ya Jipange na Pepa, Aziz Hashim amesema maandalizi yote ya kuanza kuzunguka katika shule za sekondari, ikiwemo kupatikana kwa vibali kutoka kwa wakurugenzi wa manispaa na wakuu wa shule mbalimbali yanaendelea vizuri na siku chache zijazo mpango wa kutembelea shule za Sekondari utaanza.

“Tutaanza na shule za Sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam kisha baada ya hapo tutaendelea katika shule nyingine. Lengo ni kuhakikisha tunawafikia wanafunzi wote wa sekondari nchi nzima kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuizoea mitihani na kuwa-keep busy na kusoma kwa lengo la kufaulu mitihani yao ya mwisho.

“Wanafunzi wengi wanafeli si kwa sababu hawana akili, bali ni kwa sababu hawajapata mitihani ya kutosha ya kujipima kabla ya kufanya mitihani ya taifa! Tutahakikisha mitihani inakuwa sehemu ya maisha ya wanafunzi wote ili kuwaondolea homa ya mitihani na kupanic kunakosababisha wengi wafeli,” alisema Hashim na kuongeza:

“Pia tutakuwa tukitoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi watakaokuwa wakifanya vizuri kwenye maswali ya papo kwa hapo na watakaokuwa wakifanya vizuri kwenye mitihani inayochapishwa kwenye magazeti yetu.

“Kutakuwa na zawadi kama fedha taslimu, vifaa vya shule kama madaftari, vitabu, mabegi ya shule, mathematical sets na kwa wale watakaofanya vizuri mfululizo, wanaweza kujishindia nafasi ya kipekee ya kugharamiwa masomo yao ya juu na Kampuni ya Global Publishers.”

Na Mwandishi Wetu

Leave a Comment