
ILE kiu ya Watanzania kutaka kuona siku moja katika Ligi Kuu ya England kuna Mtanzania anashiriki ligi hiyo sasa imetimia baada ya Mbwana Samatta, juzi Jumatatu kutangazwa rasmi kuwa mchezaji wa Aston Villa.
Samatta amejiunga na timu hiyo akitokea KRC Genk ya Ubelgiji ambayo alijiunga nayo mwaka 2016, akitokea TP Mazembe ya DR Congo iliyomsajili mwaka 2011 akitokea Simba iliyomsajili kutoka African Lyon (Mbagala Market).
Kocha, Jumanne Chale ambaye sasa hana timu ya kufundisha, ndiye aliyempa Samatta misingi ya soka wakati akiwa kocha mkuu wa Mbagala Market ilipokuwa Ligi Daraja Kwanza na baadaye Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo anamzungumzia Samatta kwa kusema: “Nichukue nafasi hii kumpongeza kwa mafaniko hayo makubwa aliyoyapata.

“Nakumbuka wakati nikimfundisha pale Mbagala Market, siku zote alikuwa akiniambia anapenda siku moja acheze Ligi Kuu ya England na hasa katika timu ya Manchester United.
“Nilikuwa nikimwambia asikate tamaa apambane zaidi na ajitahidi kuzingatia misingi yote ya soka ikiwemo nidhamu na kujituma mazoezini.
AZAM WATAKA KUSAJILI
“Baada ya Azam kupanda walitaka kumsajili Samatta, nilikataa na nikaenda kwa baba yake mzazi nikiwa na Jamal Kisongo, kumwambia amwache kwanza akomae. “Nashukuru Mungu, mzee Samatta alisikia ombi langu, Azam ilitaka kumsajili kwa kiasi kinachozidi Sh milioni 10 na mshahara Sh 150,000 kwa mwezi.
JINSI ALIVYOJIUNGA NA SIMBA
“Baada ya kupanda ligi kuu, Mo aliinunua timu na kuibadilisha jina na kuwa African Lyon, baada ya muda aliachana nayo na hapo ndipo Simba walipokuja kumsajili.
“Nilimwambia baba yake kuwa sasa anaweza kwenda kwani ameshakomaa, Simba walimsajili kipindi cha dirisha dogo mwaka 2010, alipofika hapo hakuwa akipewa nafasi sana ya kucheza lakini niliamini tu ipo siku ataonyesha makali yake.
“Siku aliyopewa nafasi ya kucheza ilikuwa dhidi yetu African Lyon na alitufunga mabao mawili, moja kati ya bao hilo alitoka na mpira katikati ya uwanja huku akipiga chenga na kufunga.
“Nakumbuka Simba alicheza kama mechi sita tu kisha akaondoka zake na kujiunga na TP Mazembe. “Lakini pia nimpongeze tu Jamal Kisongo kwa kumpambania Samatta.”