
Leo macho yote ya mashabiki wa soka duniani yanaelekezwa jijini Manchester, ambapo wapinzani wa jadi Manchester United na Manchester City wanakutana katika pambano kubwa la Premier League, maarufu kama Derby ya Manchester.
Mechi hiyo itapigwa katika Uwanja wa Old Trafford kuanzia saa 9:30 alasiri kwa saa za Tanzania (EAT), huku presha kubwa ikitawala pande zote mbili kutokana na historia ndefu ya uhasama, heshima ya jiji na matarajio makubwa ya mashabiki.
Derby ya Manchester si mechi ya kawaida. Ni pambano la fahari, utambulisho na ubabe wa jiji. Kwa Manchester United, huu ni mchezo wa kuthibitisha bado wana nafasi katika mbio za ushindani wa juu, huku wakihitaji ushindi mbele ya mashabiki wao ili kurejesha imani na heshima.
Kwa upande wa Manchester City, mabingwa watetezi wa ligi, wanaingia wakiwa na dhamira ya kuendeleza ubabe wao ndani ya jiji na kulinda rekodi yao nzuri dhidi ya wapinzani wao wa jadi. Kikosi cha Pep Guardiola kinatazamiwa kuonyesha soka la kiwango cha juu, umiliki wa mpira na mashambulizi ya kasi.
Historia inaonyesha kuwa mechi hizi mara nyingi huwa na ushindani mkali, mabao ya kusisimua na matukio yasiyotabirika. Licha ya tofauti ya viwango kwenye msimamo wa ligi, Derby ya Manchester mara zote hubeba sura yake tofauti, ambapo nafasi ya ubingwa, takwimu au majina makubwa mara nyingi husahaulika kwa dakika 90.
Mashabiki wanatarajia kuona burudani ya hali ya juu, mapambano ya nguvu uwanjani na matokeo yatakayozungumzwa kwa muda mrefu ndani na nje ya jiji la Manchester.

