SUPASTAA Kylian Mbappe ametoleana maneno ya shombo na kocha wake wa Paris Saint-Germain, Thomas Tuchel baada ya fowadi huyo kutolewa uwanjani kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Montpellier juzi Jumamosi.
Mbappe aliifungia timu yake bao la nne dakika ya 57 lakini alitolewa uwanjani dakika kumi baadaye, uamuzi ambao haukumfurahisha.
Mfaransa huyo alipokuwa akitoka, alikutana na kocha wake kwenye mstari, akaanza kumpa makavu kwa sekunde 15 kabla ya kuelekea kwenye benchi.
Lakini wakati akielekea kwenye benchi, kocha huyo alimshika mabegani, naye akaanza kumpa mbovu, akionekana kumueleza kuhusu uamuzi wake wa kumtoa na kulaani kitendo cha fowadi huyo kumkasirikia.
Wakati akiwa amewekewa mikono mabegani, Mbappe alikuwa akijaribu kuitoa kwa hasira lakini kocha huyo aliendelea kumkazia, hatimaye akafanikiwa kumpiga chenga na kwenda kwenye benchi akiwa amenuna.
Kinda huyu mwenye miaka 21, amefunga mabao 22 katika michezo 25 ya michuano yote msimu huu na ilionekana alitaka kuboresha rekodi hiyo katika dakika 20 za mwisho.
Tabia hiyo ya Mbappe kwa kocha wake, imewashangaza wengi kwani hakuwahi kuhusishwa na masuala yoyote ya utovu wa nidhamu.
Hiyo imekuja baada ya Mbappe kusita kusaini mkataba mpya PSG na sasa inaanza kuonekana kuwa huenda yupo njiani kuondoka klabuni hapo.
PARIS, Ufaransa
