×

Hakimu Ataka Serikali Ikamilishe Upelelezi Kesi ya Magoti

UPANDE wa mashitaka umetakiwa kukamilisha upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh. mil.  10 inayowakabili Afisa wa Kituo cha Sheria (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake mtaalamu wa mambo ya Tehama, Theodory Gyan (36).

 

Hatua hiyo inatokana na hoja zilizoibuliwa na mawakili wa utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega, baada ya Wakili wa Serikali, Renatus Mkude,  kudai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo akaomba ahirisho.

 

Wakili wa Tito, Alex Mgongolwa, amedai kuwa kiini cha kesi hiyo kimejikita katika teknolojia ya mfumo wa kielektroniki ambapo kompyuta ndiyo imetajwa na ni dhahiri kwamba upelelezi hauhitaji mambo makubwa.

 

Kutokana na hoja hiyo, Wakili Mkude amedai kuwa ni kweli kuna masuala ya teknolojia katika misingi ya mashitaka yaliyopo lakini masuala hayo yanahusisha mambo mengi ambayo mengine ili kuyapata ni lazima yatafutwe.

 

Hakimu Mtega amesema kuwa amezisikia taarifa za pande zote mbili, hivyo mahakama hiyo inauelekeza upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi katika maeneo ambayo haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi Februari 19, 2020, na washitakiwa wamerudishwa rumande.

 

Miongoni mwa mashtaka yao inadaiwa kwamba katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania,  kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani, kwa makusudi, walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahsusi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh. Mil 17,354,535.

 

Leave a Comment