×

Watanzania Tumuombeeni Bi Hindu


MAOMBI ya Watanzania yanahitajika kwa msanii mkongwe wa filamu Bongo, Chuma Suleiman ‘Bi Hindu’ ambaye kwa sasa ni mgonjwa anayesumbuliwa na bega la mkono wa kulia, Amani limeongea naye.

Akizungumza na Amani, nyumbani kwa mama yake, Magomeni Dar, Bi Hindu alisema anasumbuliwa na ugonjwa wa kusagika mifupa katika bega lake la kulia ambapo maradhi hayo yamesababisha ashindwe kufanya harakati zake za maisha na kubaki akihangaika tu kwenye hospitali mbalimbali.

Alisema kwa miezi nane sasa hawezi kufanya kazi yoyote zaidi ya kuhudhuria kwenye hospitali hizo lakini hali ya afya yake bado ni tete.

“Ugonjwa huu umenifanya niondoke kwenye nyumba yangu na kuhamia hapa kwa mama yangu kwa ajili ya kuuguzwa,” alisema Bi Hindu.

Bi Hindu alieleza kuwa sababu ya kutoka nyumbani kwake na kuhamia kwa mama yake ni kwa ajili ya kupata uangalizi zaidi wa wauguzaji.

“Nimezaa watoto kumi na moja lakini sasa nimebakiwa na watano wengine nimezika na hao watoto wengi wao wanaishi kwenye nyumba hii hapa kwa mama. Hivyo, ndiyo niliowafuata hapa kwenye nyumba ya marehemu mama yangu,” alisema Bi Hindu.

Kwa upande mwingine, mkongwe huyo wa filamu aliwashukuru, EFM Radio ambako ndiko anakofanya kazi, viongozi wa Simba SC akiwemo mfadhili mkuu wa timu hiyo, Mohammed Dewj ‘Mo’ kwa kushiriki naye katika kupata matibabu.

Licha ya kwamba bado hali yake siyo nzuri, Bi Hindu aliwaomba Watanzania wamuombee na wasiwe na wasiwasi kwani hali yake inaendelea vizuri kiasi kuliko alivyokuwa mwanzo.

Imeandikwa na Neema Adrian na Richard Bukos.

Leave a Comment