


Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo Korea (KOICA )limetoa msaada wa wataalamu 10 waliobobea katika masomo ya Sayansi na TEHAMA, kwa shule ya sekondari maalum ya mfano mkoani Arusha ya Mrisho Gambo kwa ajili ya kufundisha walimu na wanafunzi masomo hayo kwa nadharia na vitendo.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea wataalam hao mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amesema wataalam hao watakuwepo nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja na watakuwa wakitoa elimu na ujuzi huo kwa walimu wa Tanzania ili watakapoondoka waweze kuendeleza ujuzi huo ambao utazalisha wataalam hao wa baadae ambao watasaidia katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda.
Wakati huo huo wadau mbalimbali wa elimu mkoani humo wameendelea kuunga mkono jitihada za mhe Rais na mkuu wa mkoa wa Arusha kwa kuhakikisha dhamira ya kutoa elimu bure na bora nchini inatimia ambapo benki ya EXIM imekabidhi hundi ya shilingi milioni 25 kwa ajili ya kununua vitanda pacha 100 kwa ajili ya mabweni ya sekondari hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo ya mfano Afisa Mkuu wa benki ya EXIM, Jafffari Matundu amesema kama benki inatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa Tanzania hivyo wameamua kutoa fedha hizo kama ulivyo utaratibu wa benki hiyo kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii.
Naye Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. Maulid Madeni amesema watahakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa lakini pia kwa kuwa jiji lina karakana yake watasimamia vitanda hivyo vitengenezwe kwa viwango bora kabisa.
Shule ya sekondari Mrisho Gambo iliyopo kata ya Olasity jijini Arusha ina wanafunzi 144 ambao wanasoma masomo ya Sayansi na biashara .