MBUNGE David Obala kutoka Ngora Mashariki, Uganda amepeleka nzige bungeni juzi Jumanne, akilenga kupinga serikali kuchelewa kukabiliana na janga hilo ambalo linahofiwa kusababisha njaa kutokana na mazao kuharibiwa.
Serikali ya Uganda imesema imeiona video ya mbunge huyo mitandanoni na kusema imenunua lita 10,000 za kuua nzige hao kutokea angani.
Baada ya mbunge mwingine kulalamika, Obala alilazimika kuikabidhi chupa iliojaa nzige kwa afisa wa bunge anayesaidia katika kuweka amani bungeni.
Dawa iliyonunuliwa inatarajiwa kuwasili nchini humo Kesho (Ijumaa) kutoka nchini Japan. Wadudu hao wamedaiwa kusambaa katika wilaya 17 nchini Uganda zikiwemo za Acholi, Karamoja, Teso na maeneo yaliopo magharibi mwa Mto Nile.
Wilaya nyingine ni Abim, Kaabong, Nakapiripirit, Amudat, Agago, Katakwi, Nabilatuk, Moroto, Kitgun, Soroti na Kole.
