ZIKIWA zimebaki takribani siku 14 kabla ya Yanga haijacheza dhidi ya Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amesema atatumia dakika 360 kuiweka sawa timu yake kupata ushindi katika mchezo huo.
Yanga ambayo itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, itakuwa na kibarua kikubwa cha kuibuka na ushindi ili kupunguza gepu la pointi dhidi ya Simba.
Simba ambayo jana Jumamosi ilicheza dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, kabla ya mchezo huo ilikuwa kileleni na pointi 59, huku Yanga ikiwa nafasi ya nne na pointi zake 40.
Yanga kabla ya kucheza dhidi ya Simba, hapo kati itacheza mechi nne ambazo ni sawa na dakika 360.
Mechi hizo ni dhidi ya Coastal Union itakayochezwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kisha dhidi ya Gwambina katika Kombe la FA. Baada ya hapo ni dhidi ya Alliance na Mbao zikiwa za ligi kuu.
Katika mechi hizo, ndizo Luc alizozitenga kwa ajili ya kujiandaa na Simba akiamini kwamba vijana wake watakuwa fiti kuibuka na ushindi na kuifukuzia kwa ukaribu Simba kileleni, hatimaye kuishusha.
“Kitu kikubwa ambacho kipo mbele yetu ni kuona tunarudisha morali ya timu kwa kuanzia mechi yetu na Coastal kwa sababu ndiyo mchezo uliopo mbele yetu na ushindi ndiyo jambo ambalo kila mmoja anataka kuliona kutokana na matokeo ya mechi zetu za nyuma.
“Unajua baada ya Coastal bado tutakuwa na mechi tatu ambazo zote ushindi ndiyo lengo kubwa kabla ya kucheza na Simba, sasa jambo muhimu kwetu ni kuona mikakati na mipango yetu inakwenda sawa kulingana na matokeo yaliopita ambayo kwetu hayakuwa mazuri,” alisema Eymael.

