NAIBU Waziri wa Afya nchini Iran, Iraj Harirchi, ambaye amekuwa mstari wa mbele nchini humo katika kupambana na Corona Virus amegundulika kuambukizwa virusi hiyo.
Msemaji wa wizara hiyo amethibitisha hayo alipokuwa anafanya mahojiano na chaneli ya runinga ya taifa na kusema waziri huyo amewekwa sehemu maalumu ya uangalizi.
Aidha, Jumatatu iliyopita Shirika la Habari nchini humo lilisema watu 50 wamefariki kwa virusi hivyo huku likieleza kuwa linapendelea kutoficha mambo kuhusu Corona kwani yanahusisha maisha ya watu.
Hata hivyo, Harirchi alipinga taarifa hiyo akisema atajiuzulu ikiwa hata nusu ya idadi iliyotajwa (watu 50) watafariki dunia kutokana na Virusi vya Corona.
Taarifa kutoka Ikulu zilithibitisha maambukizi ya kwanza ya virusi hivyo nchini humo Jumatano iliyopita huku Wizara ya Afya ikisema watu wawili wameambukizwa na wametengwa.
