KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, amefunguka kwamba alitumia mbinu ya kuwatazama Gwambina wakati walipocheza na Simba, mwaka jana kisha akapata nafasi ya kuwamaliza walipokutana nao juzi katika mechi ya Kombe la Shirikisho (FA).
Eymael, raia wa Ubelgiji, amesema kwamba alitumia video hizo wakati Gwambina walipocheza na Simba katika mechi ya kirafiki ya kuzindua uwanja wao mwaka jana ambapo Simba walishinda kwa penalti 4-2.
Kocha huyo juzi Jumatano aliiongoza Yanga kuwatupa nje Gwambina iliyo Daraja la Kwanza kwa kuifunga bao 1-0 katika mechi ya FA iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Eymael alisema: “Niliisoma Gwambina katika video yao walipocheza na Simba, mwaka jana kwa sababu sikuwa nawajua kabla ya kucheza nao. Ni timu nzuri ambayo ina wachezaji wenye uzoefu wa kucheza ligi kuu na wanacheza soka zuri.
“Unajua unapocheza na timu ambazo ziko madaraja ya chini zinakuwa na mbinu nzuri juu yenu, siyo hapa tu hata Afrika nzima wanakuwa hivyo, lakini kitu kizuri ni kwamba sisi kwetu kila mmoja alifanya kazi yake vizuri, ndiyo maana tukashinda mchezo huu na kusonga mbele kwa sasa,” alisema Eymael.
Stori na Said Ally, Dar es Salaam

