MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, jana aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamatwa na kuhojiwa katika kituo cha Polisi cha Bomang’ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa zaidi ya saa mbili.
Mbunge huyo wa Hai alikamatwa jana (Ijumaa) Februari 28, 2020, saa 12 jioni baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Nkoromu kata ya Masama Kati wilayani Hai.
Alihojiwa kuanzia saa 12:35 jioni hadi saa 3:20 usiku na alipotoka baada ya dhamana aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hawezi kuzungumza chochote.
“Mbowe alikamatwa baada ya kutuhumiwa kusema au kutoa maneno yanayoashiria uchochezi, kuamsha hisia na chuki dhidi ya serikali na polisi. Amehojiwa na baada ya mahojiano alipewa haki ya dhamana,” amesema kamanda Hamdun
Katika mkutano huo, Mbowe amesema hawezi kupongeza utendaji kazi wa serikali mpaka atakapokuwa na uhakika serikali inatenda haki kwa watu wote.
Alikamatwa muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara saa 11:58 jioni
Wakati akijiandaa kuondoka eneo hilo, polisi walikwenda katika gari lake wakieleza kuwa wanamhitaji kituoni, ombi ambalo liliridhiwa na mwenyekiti huyo baada ya mvutano uliodumu takribani robo saa.
Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni awali aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa amemwandikia barua Rais John Magufuli kutaka uchaguzi wa serikali za mitaa urudiwe nchi nzima.
“Nimemuandikia rais barua nimemwambia Chadema kama chama kikuu cha upinzani hawawatambui wenyeviti wa serikali za mitaa waliochaguliwa, tunahitaji uchaguzi urudiwe nchi nzima ili wapatikane viongozi waliochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi,” alisema Mbowe.
