×

Serikali Yaimarisha Ulinzi Simba,Yanga

KUELEKEA mechi ya watani wa jadi Yanga dhidi ya Simba, Serikali ya Tanzania imeamua kuboresha ulinzi marudufu ili kudhibiti usumbufu unaoweza kujitokeza.

 

Kumeandaliwa mageti maalumu ya kupita wageni rasmi, waandishi wa habari, huku wale mashabiki wa kawaida wakiachiwa uhuru wa kupita kwenye mageti yote kuzunguka uwanja huo.

 

Barabara zote zitafungwa, ikiwemo ile ya Chuo Kikuu cha Elimu (Duce) kuja Taifa, ambapo barabara moja tu pekee, ile ya kutokea bandarini kuelekea Ubungo ikiwa wazi, huku magari yenye kadi maalumu ndiyo yatakayoruhusiwa kupita na kuingia uwanjani.

Magari ya askari yatatanda kuzunguka uwanja wote, huku askari wakimwaga kila kona kwa lengo la kudhibiti mashabiki wenye nia hovu na kutaka kuanzisha vurugu za aina yoyote.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana Alhamisi, Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Yusuph Singo alisema wameamua kuboresha ulinzi marudufu kwa lengo la kuzuia vurugu na ghasia ambazo zinaweza zikaharibu ubora na ukubwa wa mchezo huo.

 

“Awamu hii tumejipanga na kuboresha ulinzi zaidi ya ilivyokuwa awali ili kuwapa nafasi mashabiki kushangilia kwa amani na kudhibiti wale wote wenye nia hovu, niwaombe mashabiki kuja uwanjani mapema na kuingia kwa kufuata utaratibu,” alisema.

Stori: Ibrahim Mussa na Issa Liponda

Leave a Comment