KIMYA kimetawala mjini kwa mashabiki wa Simba, baada ya jana kushuhudia timu yao ikichapwa bao 1-0 na Yanga katika matokeo ambayo hawakuyatarajia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.
Hii ni mara ya pili, Simba wanadhalilika mbele ya Rais, baada ya misimu kadhaa iliyopita kufungwa na Kagera Sugar bao 1-0 kwenye uwanja huohuo wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kabla, na rais akawachekesha watu aliposema “wametobolewa tundu.” Hiyo ndiyo ilikuwa mechi pekee Simba wanapoteza msimu huo, ingawa walibeba ubingwa.
Msimu huu tayari Simba ilikuwa imeshapoteza michezo miwili kabla haijakutana na Yanga jana.
Mghana Bernard Morrison ndiye aliyewainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bonge la bao dakika ya 43 kwa shuti kali la faulo ya moja kwa moja, lililotokana na yeye mwenyewe kuchezewa rafu na kiungo Jonas Mkude.
Yanga waliuanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza tu walipata kona iliyopigwa fupi kwa Morrison aliyepiga krosi ambayo ilimpita kwa nyuma kiungo Ditram Nchimbi.
Lakini dakika ya 6, Clatous Chama alipiga krosi akipokea pasi ya Luis Miquissone lakini Metacha Mnata akapangua.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa katika dakika 10 za kwanza, timu hizo zikishambuliana kwa zamu. Lakini Yanga walionekana kuwa bora zaidi katika dakika hizo kutokana na kutengeneza nafasi nyingi. Dakika ya 11, Nchimbi alipiga shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari, likatoka nje ya lango baada ya kupokea pasi ya Juma Abdul.
Dakika ya 14, Yanga walikosa bao baada ya Nchimbi kupiga krosi ya chini ambayo ilidakwa na kipa Manula.
Dakika ya 18, Nyoni alikaa chini akiashiria kuwa ameumia lakini alitibiwa na kurejea uwanjani. Dakika ya 20, Yanga walipata kona ya pili ambayo haikuwa na madhara kwa Simba.
Kumbe Nyoni aliumia, kwani hakuweza kuendelea na mchezo, alitoka dakika ya 22 na nafasi yake ikachukuliwa na Kennedy Juma.
Dakika ya 24, Nchimbi alikosa tena bao baada ya kugongana na mpira akiwa ndani ya 18, kufuatia pasi ya chini ya Jaffar Mohammed.
Dakika ya 26, kiungo wa Simba, Jonas Mkude alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea faulo ya makusudi Morrison wakati mwamuzi tayari alikuwa ameshapuliza filimbi.
Morrison aliwafurahisha mashabiki wa Yanga baada ya kukanyaga mpira mbele ya Shomari Kapombe.
Simba nusura wapate bao dakika ya 29 wakati Luis alipopiga shuti kali lililopanguliwa na Metacha lakini mpira ukabaki kwenye eneo la hatari, ukakutana na Bocco, ambaye naye alipiga shuti, Metacha akapangua tena, kisha mabeki wakaokoa hatari hiyo.Simba walipata kona ya kwanza dakika ya 36, baada ya Makapu kuutoa mpira nje.
Dakika ya 39 Simba walikosa nafasi nyingine ya goli baada ya Meddie Kagere kupiga shuti lililogonga mwamba na mpira kurejea uwanjani, ukamkuta Luis ambaye alipiga shuti jingine lililopanguliwa na Metacha.
Dakika ya 47 kipindi cha kwanza, Kagere alikosa tena bao baada ya shuti lake kupanguliwa na Metacha, inakuwa kona lakini haina madhara.
Kipindi cha pili kilipoanza, dakika ya 50, Morrison alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuunganisha mpira wa krosi wa Jaffar.
Morrison alitoka uwanjani baada ya kuumia, na nafasi yake ikachukuliwa na Patrick Sibomana, aliyeingia moja kwa moja na kupiga faulo inayookolewa na mabeki wa Simba na kuwa kona.
Dakika ya 61, Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Kahata na nafasi yake ikachukuliwa na Deo Kanda.
Lakini dakika moja baadaye, Nchimbi alikosa bao la wazi baada ya kufanikiwa kumtoka beki Pascal Wawa, akabaki na kipa Manula, akapiga pasi iliyokosa wamaliziaji waliochelewa.
Dakika ya 69, Simba walimtoa Meddie Kagere na nafasi yake ikachukuliwa na Hassan Dilunga. Dakika ya 86, Yanga anatoka Balama na kuingia Deus Kaseke.
Matokeo hayo yameifanya Yanga ipande hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 25. Simba bado ipo kileleni ikiwa na pointi 68, lakini ina michezo miwili mbele ukilinganisha na Yanga. Kama Yanga akishinda viporo vyake viwili, atabakiza pointi 12 kabla ya kuwafikia Simba.
Dakika ya 91, Kaseke alikosa bao baada ya shuti lake kugonga mwamba kutokana na pasi nzuri ya Sibomana. Lakini dakika moja baadaye, Kennedy alipiga shuti lililokwenda nje kidogo ya lango.
METACHA ATISHA KWA KUOKOA
Kipa wa Yanga, Metacha Mnata aliwafurahisha mashabiki wengi wa Yanga, akiwemo kocha wake Luc Eymael kutokana na kuokoa hatari nyingi sana za washambuliaji wakali wa Simba.
Kipa huyo alifanya kazi kubwa ya kuokoa mara mbilimbili mashuti ya washambuliaji wa Simba na mwishoni mwa mchezo, aliokoa hatari nyingine ambayo ingeweza kusababisha madhara.
SIMBA WASHINDWA KUAMINI KILICHOTOKEA
Wachezaji wa Simba hawakuamini kilichotokea baada ya dakika 90 za mpambano huo kumalizika na walionekana wakiwa wamenyong’onyea sana.
Pia mashabiki wao walikuwa kimya jukwaani huku wengi wao wakiwa wameweka mikono yao kichwani kwa huzuni.
SVEN AFUNGUKA
Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck alisema baada ya mchezo: “Siwezi kuwalaumu wachezaji wangu kwa kuwa walicheza vizuri na walionyesha kupambana kwa nguvu zote. Tulianza vizuri katika dakika za mwanzo kuanzia dakika ya 15, 20 kwa kuwa tulikuwa na muunganiko mzuri lakini hadi mapumziko tulikuwa nyuma kwa bao 1-0. Nawashukuru wachezaji ingawa hatuna nafasi ya ubingwa msimu huu kutokana na kuachwa mbali.”
LUC AFUNGUKA
Kwa upande wake Kocha wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael alisema ana furaha kwa kuwa amewafunga wapinzani wazuri.
“Tumecheza Dabi kwa shauku kubwa ya kushinda kwa kuwa inakuwa ni kama fainali na ndivyo tulivyofanya, lakini kwa upande wa Metacha, amefanya kazi kubwa kutokana na mipira aliyoiokoa.
PASI ZA YANGA VS SIMBA
Katika mchezo huo, Yanga walipiga jumla ya pasi 167, kati ya hizo ni 11 tu ndizo zilizoharibika, wakati Simba walipiga pasi 178 lakini zilizoharibika zilikuwa ni 44. Hivyo Yanga walipiga pasi nyingi zaidi sahihi ambazo ni 156, ukilinganisha na Simba waliopiga pasi sahihi 134.
Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohammed, Lamine Moro, Juma Makapu, Papy Tshishimbi, Mapinduzi Balama, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Bernard Morrison.
Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Luis Miquissone, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata.
IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam
