
KOCHA wa zamani wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems amefunguka licha ya timu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu Bara lakini haoni nafasi yao ya kuweza kuvunja rekodi ya kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.
Aussems ametoa kauli hiyo wakati Simba inaelekea kutetea ubingwa wa ligi kuu kufuatia kuongoza ligi ikiwa na pointi 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Aussems alisema kuwa kufanya vizuri kwenye ligi kwa timu hiyo hakuwezi kutoa picha ya wao kuweza kuvunja rekodi ya msimu uliopita kwenye michuano ya kimataifa kutokana na siasa za viongozi wa timu hiyo.
“Najua malengo yao ni kuona wanafanikiwa kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao na hilo limewezekana kwa kuwa wao ndiyo wanaongoza ligi hadi sasa lakini pia wamewaacha mbali wapinzani wao, Azam na Yanga.
“Lakini ubora wao kwenye ligi haumaanishi ndiyo sababu ya wao kuweza kufikia malengo ya kimataifa kama msimu wa mwaka juzi, hilo haliwezi kutokea kwa sababu siasa za viongozi na kila mmoja atahitaji kuona cha kwake ndiyo sahihi na ugumu wa michuano kimataifa kwa timu zenye malengo upo wazi ila siyo Simba hii,” alisema Aussems.
