×

Ummy: Hakuna Mgonjwa wa Corona Hospitalini Mawenzi

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  leo Machi 14, 2020, amewatoa hofu Watanzania kuwa hadi nchi haina mgonjwa wa maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) baada ya wasiwasi wa kuwepo abiria wenye maambukizi hayo  katika Hospitali ya Mawenzi, Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Machi 14, 2020, na wizara, imesema kwamba  Machi 13, 2020  asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) walipokelewa wasafiri sita wakitokea Kenya, wawili ni raia wa Denmark na wengine wawili wa Norway (wanawake watano na mwanamme mmoja) ambapo baada ya ukaguzi mmoja alikutwa na homa, kikohozi na mwili kuchoka.

Wasafiri wote sita walitengwa katika Hospitali ya Mawenzi na kuchukuliwa sampuli zao ambazo zilipelekwa maabara Dar es Salaam, na uchunguzi umebaini wote hawana maambukizi.  Msafiri aliyekutwa na joto kali amebainika kuwa na mafua ya kawaida, wote wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao.

”Ninawatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa Tanzania haina mgonjwa mwenye maambukizi ya virusi vya Corona, ninapenda kuendelea kuwataka wananchi wachukue tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu, pia natoa rai kwa watu kutosambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa na serikali,” amesema waziri huyo katika taarifa hiyo.

Leave a Comment