
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kitendo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vincent Mashinji kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaokoa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliohukumiwa hivi karibuni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya Hakimu Mkuu wa Kisutu, Thomas Simba.
Dk. Mashinji ambaye alikuwa mmoja wa watuhumiwa katika kesi hiyo ya uchochezi pamoja na viongozi wengine wanane wa Chadema akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Machi 10 mwaka huu walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela au kulipa faini ya Sh milioni 350.
Prof. Lipumba ambaye leo Machi 14, 2020 ametembelea Ofisi za makampuni ya Global Group na kufanya mahojiano katika kipindi maalum na +255 Global Radio na Global TV Online na kueleza kuwa haijulikani kama ni mkakati wa CCM au Chadema, Dk. Mashinji kuhamia chama tawala, kiujumla umewaokoa viongozi hao.
“Pamoja na kwamba mahakama imehukumu ila rais ametoa mchango, sasa unastaajabu imetumia gharama kubwa kuendesha kesi, lakini mnatumia fedha kuwatoa watuhumiwa haohao,” alisema.

Aidha, akizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Profesa Lipumba alisema yupo tayari kuungana na vyama vingine vya upinzani ila kwa utaratibu maaalum.
Alisema kwa upande wa uchaguzi wa Zanzibar chama hicho kinaamini kuwa na wagombea imara wenye uwezo wa kukisimamisha chama hicho tofauti na watu wanavyotafsiri.
“Wazanzibar wanaounga mkono CUF wakati kinaanzishwa walilishana yamini, kwamba ndiyo chama cha ukombozi, atakayeondoka mwenyezi Mungu amlaani.

“Kwa hali ilivyo wananchi wa Pemba wanajua mchango wangu, kwamba Wanzazibar wawe na haki sawa na Tanzania wengine.
“Tunao viongozi imara kama Halifa Suleiman Halifa. Musa Hadji waliosajili chama na wanatuunga mkono, si kwamba hatuna watu upande wa Zanzibar wenye kutuunga mkono,” alisema.

Aliongeza kuwa si kweli kwamba wabunge wa CUF waliosalia ndani ya chama hicho kwa sasa wamepanga kuhamia vyama vingine ikiwamo ACT, kama ambavyo taarifa zinazagaa mitandaoni.
Pamoja na mambo mengine alisema ili ipatikane tume huru ya uchaguzi pamoja na kutekeleza lengo la upatikanaji wa katiba mpya, lazima chama tawala kitoke madarakani.

“Katika nchi nyingi za Kiafrika katiba mpya inapatikana baada ya chama tawala kutoka madarakani, mfano Kenya chama cha KANU kiliangushwa, Zambia, Unip kilianguka, Malawi, Malawi Congress Party kilianguka. Tuna kazi kubwa kuleta mabadiliko wakati chama tawala kikiendelea kutawala,” alisema.

