Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Majaliwa amesema pia michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili, michezo ya shule za msingi na sekondari (UMITASHUMTA na UMISETA) na ile ya mashirika ya umma, imesitishwa kuanzia leo kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Kuhusu kufungwa shule, amesema wizara husika itafanya marekebisho ya ratiba ya wanafunzi kidato cha sita, ambao wanatarajiwa kufanya mitihani tarehe 4 mwezi wa tano kwani watakuwa na muda mfupi. Kwa hiyo tarehe zitasogezwa mbele ili wapate nafasi ya kusoma, ” amesema Mjaliwa akiongea na wanahabari jijini Dodoma.
Pia alieleza kwamba serikali imeshamweka chini ya uangalizi maalum mgonjwa alyebainika kuwa na ugonjwa wa Corona nchini na amewahakikishia wananchi kwamba serikali inaendelea kuwafuatilia watu alioshirikiana nao tangu alipoingia nchini na tayari wapo ambao wamewekwa kwenye karantini kwa siku 14 na sampuli zao zimechukuliwa ili kupimwa.
“Tumeagiza Wizara ya Mambo ya Ndani isimamie mipaka yetu ili wanaoingia watumie mipaka rasmi, wanaosimamia sehemu za mikusanyiko kama benki na stendi za mabasi wahakikishie sabuni maalum aina ya ‘Sanitizer’ zinatumika na serikali itachukua hatua kwa wanaopandisha bei ya sabuni hiyo na vifaa vya kujilinda,” alisema Majaliwa.
Kwa habari zaidi tazama video hapa chini.
