MUFTI wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi, amewaagiza walimu wa madrasa kufunga madrasa zote hadi utakapotangazwa utaratibu mpya. Aidha amewataka waumini wote kuchukua udhu nyumbani wanapokwenda msikitini, ikiwa ni tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Akizungumza leo Jumatano Machi 18, na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, amesema agizo hilo linapaswa kutekelezwa haraka iwezekanavyo na kwamba taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Kuhusu swala ya Ijumaa na ile ya Jamaa, alisema zitaruhusiwa kwa sasa na huenda itabadilishwa kulingana na mazingira ya ugonjwa huo.
“Kuanzia sasa swala za Jamaa zinapaswa kuswaliwa kwa kuachiana nafasi na kuzingatia usafi ili kupunguza maambukizi,” amesema.
Kwa maeneo ambayo yanashukiwa wa ugonjwa huo na yamewekwa karantini, amesema hairuhusiwi kuendelea na swala hizo kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kuwa ni dhambi kumuambukiza ugonjwa mwenzio kwa makusudi.
Amesema Muislamu yeyote atakayepata maradhi haya ni haramu kwake kuhudhuria swala za Ijumaa na Jamaa kama ambavyo ni haramu kwake kuchanganyika na wengine kwani kufanya hivyo ni kuusambaza na kueneza ugonjwa huo kwa wenzake.
