MTANGAZAJI maarufu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Salim Kikeke, amefunguka maisha aliyoyapitia kabla ya kuwa mtangazaji mkubwa akiiwakilisha Tanzania barani Ulaya na dunia nzima kwa jumla.
Akipiga stori na Kituo cha Radio cha +255 Global Radio na Global TV online, leo Ijumaa, Machi 20, 2020 alipotembelea katika ofisi za Global Group, Kikeke amesema alipomaliza kidato cha sita alikwenda kusomea kilimo lakini baada ya kuhitimu masomo yake alikosa ajira jambo ambalo lilimfanya abadilishe mwelekeo na kuanza kutafuta njia za kuingia kwenye tasnia ya habari.
“Niliamka siku moja nikaamua kwenda kwenye vyombo vya habari kuomba ajira ya utangazaji, nilifika ITV na kuonana na Mkurugenzi nikamweleza ndoto yangu ya utangazaji, nilizungumza naye mambo mengi, nikaenda Channel 10, napo nikafanya hivyohivyo. Wakati huo sikuwa na elimu yoyote ya uandishi wala fani yoyote ya habari.
“Baadaye nilipata nafasi ya kazi pale CTN, kazi yangu ikawa kubadilisha kanda za muziki, niliendelea hivyo baadaye nikasomea uandishi na hatimaye nikawa nasoma taarifa za habari. Nimepita kwenye vyombo mbalimbali hapa nchini ikiwemo ITV na TBC zamani Radio Tanzania kabla ya kwenda Uingereza na kujiunga na BBC,” amesema Kikeke.
Kuhusu maisha ya London na Uingereza kwa jumla, Kikeke amesema mwanzoni alipata ugumu lakini kwa sababu alikuwa amedhamiria kufanya kazi hiyo popote pale duniani, alilazimika kuendana na mazingira ili afanye kazi yake kwa ufasaha na kupata mafanikio aliyonayo kwa sasa.
Aidha, akizungumzia mchango wake kwa Klabu ya Simba kama Balozi wa Klabu hiyo nchini Uingereza na Bara la Ulaya kwa ujumla, Kikeke amesema kazi kubwa anayoifanya ni kuitangaza Simba SC kimataifa, pia kutengeneza mahusiano na vilabu vingine vya soka nchini humo ili kubadilishana uzoefu, wachezaji na mambo mbalimbali yahusuyo soka kwa lengo la kukuza mchezo huo katika
“Nimeshazungumza na vilabu vya Ligi Kuu ya Uingereza na vingine vya Championship, lengo ni kutengeneza uhsuiano mzuri na Simba SC pamoja na kukuza vipaji ndani ya klabu hiyo. Zaidi ni kupanua wigo wa masuala mbalimbali ya soka kati ya Simba na vilabu vya Uingereza,” amesema.
Akizungumzia suala la usajili wa Mbwana Samatta anayekipiga katika Ligi Kuu ya Uingereza kunako klabu ya Aston Villa, Kikeke amesema Mtanzania huyo amepokelewa vizuri sana hapo Aston Villa na kwamba wanamkubali kuliko kawaida.
“Ni mara chache sana kwa mchezaji kusajiliwa katika dirisha dogo ana akafanya vizuri na kukubalika katika kikosi na kwa mashabiki, lakini Samatta amekuwa miongoni mwa wachezaji wachache waliokubalika Aston Villa licha ya kuingia katikati ya msimu.
“Ni mchezaji anayejituma sana, na nimeuliza kwenye maduka ya Aston Villa, Samatta ndiye anaongoza kwa kuuza jezi zake. Unaweza kuona namna ambavyo wanampenda na wana imani naye kwamba ataisaidia timu kufikia malengo.
“Nilipokutana naye nilimwambia mimi nitakuwa msitari wa mbele kumtangaza, wala sioni haya, kwa sababu nafasi aliyoipata ni ya muhimu sana kwake na taifa letu kwa ujumla, tutahakikisha tunamtangaza na kuitangaza nchi yetu hasa katika masuala ya utalii na mambo mengine mazuri yaliyopo Tanzania,” alisema.
Akimalizia kujibu swali iwapo ana mpango wa kurejea nchini kuja kufanya kazi zake huku, Kikeke amesema; “Nitarejea Tanzania huenda mwaka huu au miaka 10 ijayo, kwa sababu hapa ni nyumbani na ninatamani kuendelea kukuza vijana wengi kwenye tasnia hii adhimu kwa taifa letu.”
Kikeke ambaye anatangaza Dira ya Dunia ya BBC nchini Uingereza, kwa sasa yupo mapumziko hapa nchini kabla ya kurejea tena Uingereza kuendelea na shughuli zake.









