NAIBU Waziri Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, ameahidi ushirikiano na msanii wa Bongo Fleva nchini, Rashid Abdallah maarufu kama Chid Benz.
Shonza ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma alipofanya kikao na msanii huyo ambapo Chid alimhakikishia kuwa kwa sasa amebadilika na anataka kuwaonyesha Watanzania amefanikiwa kujikwamua katika matumizi ya madawa ya kulevya na hataki tena kurudi huko kwani ana zaidi ya miezi mitatu sasa hajatumia madawa hayo kabisa.
“Kati ya wasanii wenye kukubalika na mashabiki zao wewe ni mmoja wao na mashabiki zako ni wengi, hivyo ningependa kukuona kwanzia sasa unalijenga zaidi jina lako kwa kuonyesha kuwa umebadilika, katika kipindi hiki nitafurahi zaidi kukuona unasonga mbele na hurudi tena katika matumizi ya madawa ya kulevya. Wizara ipo pamoja na wewe kukusaidia wakati wowote ,” alisema Shonza.
Naye Chid alieleza kuwa kwa sasa hatarudi nyuma tena sababu tayari amekwishaacha kutumia madawa hayo.
“Ninaelewa bahati haiji mara mbili lakini kwangu naiona imekuja zaidi ya mara moja kwa maana ya kuwa nimekuwa naanguka nainuka, narudi kwa mashabiki wananipokea na kuendelea kukubali muziki wangu. Hakika najiona ni wakati wa kuwafurahisha zaidi mashabiki na sitawaangusha.
“Ombi langu kwa serikali ni kupata ushirikiano na mapema wiki ijayo ninatarajia kutoa wimbo wangu mmoja uitwao Beautiful ambao nimeuimba nikisifu uzuri wa mwanamke na kufuatia janga la Corona ninamwahidi mheshimiwa naibu waziri kuwa nitatunga wimbo kwa ajili ya Corona,” alisema.
Pamoja na hayo Chid alitoa wito kwa Watanzania kuacha kufanya mzaha katika mitandao ya jamii kuhusu suala la ugongwa unaoletwa na virusi vya Corona kwa sababu ni tatizo linalosumbua dunia kwa sasa, hivyo jambo la msingi ni kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali kutoka kwa wataalamu wa afya.
