×

Morrison Asani Miaka Miwili Yanga, Azima Tetesi za Simba

TETESI za Simba kumuwania kiungo mshambuliaji Mghana, Bernard Morrison zimezimwa jana baada ya staa huyo kurejesha mkataba wake wa miaka miwili pale Yanga.

 

Awali kulikuwa na taarifa kuwa, mchezaji huyo anawaniwa na Simba na ilibaki kidogo asaini huko lakini Yanga kupitia mitandao yake ya kijamii jana ilituma picha ya Morrison akiwa ameshika mkataba wake sambamba na Injinia Hersi Said kutoka GSM ambayo imekuwa akiisaidia Yanga.

 

Lakini kabla ya kurejesha mkataba huo jana, juzi usiku zilisambaa taarifa za Morrison kwenda Simba jambo ambalo lililowapa hasira viongozi wa Yanga hivyo wakapanga kwenda kushtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Awali, Mghana huyo alitua nchini na kusaini mkataba wa miezi sita ya kuichezea Yanga, lakini taarifa zinaeleza kuwa yalifanyika mazungumzo ya kumuongeza mkataba mwaka mmoja na nusu ili ikamilike miwili kamili huku tetesi zikienea kuwa bado hajaongeza.

 

Morrison alijiunga na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael kupendekeza asajiliwe ili akiongezee nguvu kikosi hicho katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, uongozi wa Yanga ulishtukia jitihada kubwa zinazo daiwa kufanywa na Simba huku wakiwatahadharisha watapeleka malalamiko TFF kama wakiendelea kumsumbua mchezaji wao.

 

“Morrison amekuja Yanga kutokana na ushawishi wa kocha Eymael ambaye ameweka bayana kuwa anamuhitaji sana mchezaji huyo, mwishoni mwa msimu ataongeza nyota wengine ambao pamoja naye wataiongezea nguvu Yanga.

 

“Hivyo, hicho wanachoendelea kukifanya Simba ni sawa na bure kupoteza muda wao kumfuata Morrison kwa ajili ya kumshawishi ili asaini huko kitu ambacho ni kigumu siyo rahisi kama wanavyofikiria.

 

“Kikubwa viongozi wa Yanga wanataka kwenda kushtaki TFF kwa kuhofia kumtoa mchezoni wakati hivi sasa akili yake ipo Yanga.” Akizungumzia ishu ya kutakiwa na Simba, Morrison alisema: “Mimi bado mchezaji halali wa Yanga mwenye mkataba, kingine ninafurahia maisha niliyoyakuta hapa tangu nilipofika nchini nikicheza mechi yangu ya kwanza na Singida United.

 

“Kiuweli hiki ambacho nimekikuta Yanga kwangu ni kipya, nimecheza kwenye nchi za Afrika Kusini, Congo na nyumbani Ghana lakini sijawahi kukutana na mapenzi mazuri ya mashabiki kama niliyoyakuta Yanga, kiukweli nayafurahia sana.

 

“Tukiwa safarini kuelekea Lindi kucheza na Namungo, basi letu lilisimamishwa mara kadhaa na kushangiliwa na mashabiki, nilishangaa zaidi zawadi ya kuku wanne niliopewa, hapa nyumbani ninapoishi nikitoka nje ninanunuliwa chakula, vitu vya thamani na makundi ya watu kunisimamisha, ni hali ya kipekee katika soka la Tanzania. Nafurahia sana maisha ya hapa,” alisema Morrison.

 

Makamu Mwenyekiti wa Yanga Frederick Mwakalebela hivi karibuni kwa kupitia gazeti hili alithibitisha kufuatwa na mmoja wa mawakala aliyetumwa na viongozi wa Simba akiomba imsajili nyota huyo kwa ajili ya kumtumia kwenye michuano ya kimataifa.

Imeandikwa na Wilbert Molandi, Musa Mateja na Said Ally

MOLINGA, YKPE WANATABIRIWA KUONDOKA YANGA / MORRISON AACHWA…

Leave a Comment