×

Majaliwa Aonya Upotoshaji Taarifa za Ugonjwa wa Corona

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo Jumamosi, Machi 21, 2020 ameonya kuhusu upotoshwaji na utoaji holela wa taarifa kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababisha na virusi vya corona (COVID 19) unaofanywa na watu mbalimbali nchini.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wakuu wa mikoa yote nchini, makatibu tawala wa mikoa na waganga wakuu wa mikoa kwa njia video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Amesema kuanzia sasa taarifa hizo zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ikilazimika zitatolewa na Waziri Mkuu na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha mikanganyiko.

 

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ifuatile watu wote wanaofanya upotoshaji kwa kupitia mitandao ya kijamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Waziri Mkuu amesema licha ya hali ya maambukizi ya corona nchini kutia matumaini, viongozi wa mikoani hawana budi kupeana taratibu za namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanawafuatilia na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote watakaobainika kuongeza bei kwa bidhaa ambazo zinatumika katika udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa corona.

 

Kuhusu viongozi wa dini, Waziri Mkuu amewaomba waendelee kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari za ugonjwa huu. Pia awaendelee kuliombea taifa.

Leave a Comment