×

Kakolanya ‘Auzwa’ Nje ya Nchi

GOLIKIPA wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Ivo Mapunda, amemshauri kipa wa Simba, Beno Kakolanya kwenda kutafuta changamoto nje ya nchi ili kulinda kipaji chake alichonacho cha kuokoa michomo golini.

 

Kakolanya alijiunga na Simba kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Yanga baada ya mkataba wake wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo kumalizika.

 

Kipa huyo tangu ametua kujiunga na Simba, amekuwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku akimuachia Aishi Manula ambaye ndio pendekezo la kwanza la Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mapunda alisema kuwa Kakolanya ni kati ya makipa bora nchini ambaye anaamini kama akitoka kwenda kucheza nje ya nchi, thamani yake itaongezeka tofauti na ilivyo hivi sasa.

 

Mapunda alisema kitendo cha kipa huyo kuendelea kukaa benchi kutasababisha yeye kiwango chake kushuka, hivyo ni wakati wa yeye kutoka hapo na kwenda kucheza nje.

 

“Binafsi Kakolanya ni kati ya makipa bora kabisa kwangu lakini tatizo hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo baada ya kukutana na ushindani wa namba kutoka kwa Manula.

 

“Ni wakati wa yeye kupiga hesabu vizuri na kuondoka hapo na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, hilo linawezekana kwake kabisa kutokana kiwango kikubwa alichonacho.

 

“Alitoka Yanga akiwa katika kiwango bora na kufanikiwa kujihakikishia nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hivyo ni suala la kuamua abaki au aondoke,” alisema Mapunda.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment