UONGOZI wa Yanga kwa kushirikiana na wadhamini wao, Kampuni ya GSM, umetaja kigezo cha mchezaji anayetakiwa kuvaa jezi ya klabu hiyo katika msimu ujao.
Kigezo kikubwa lazima mchezaji awe anacheza kwenye kikosi cha kwanza kwenye timu yake anayotokea, lakini pia timu yake ya taifa.
Hiyo ina maana kuwa, usajili wa kiungo wa Simba, Said Ndemla kutua Yanga huenda usikamilike kwani kiungo huyo hana nafasi kwenye kikosi cha Simba wala Taifa Stars.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injia Hersi Said, alisema wamepanga kutengeneza kikosi imara cha Yanga kitakachokuwa tishio kuanzia waliopo uwanjani, hadi wa benchi.
Hersi alisema kuwa hilo la usajili linawahusu wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi bila kuangalia ukubwa wa jina au umaarufu wake, hivyo hawataki kuharibu, watahakikisha wanasimamia kwa umakini kwa kushirikiana na benchi la ufundi ambalo lipo chini ya Kocha Mkuu, Mbelgiji Luc Eymael aliyefanikisha usajili wa Mghana, Bernard Morrison.
“Wengi wanajua kuwa sisi GSM ndiyo tunasajili, ukweli ni kwamba sisi kama wadhamini kazi yetu ni kufanya mazungumzo ya dau la usajili na mshahara wa mchezaji pekee.
“Baada ya mazungumzo kwenda vizuri, basi kama mdhamini tunatoa pesa lakini suala la kuandaa mikataba lipo kwa uongozi na mapendekezo yote ya usajili yanatoka kwa kocha.“Kocha mwenyewe tulishamwambia malengo yetu ya msimu ujao ni kuhakikisha tunachukua ubingwa wa ligi, hivyo usajili wake lazima ukidhi viwango kama vile mchezaji atakayekuja siyo yule wa aliyekuwa anakaa benchi katika timu aliyotokea.
“Kila mchezaji atakayesajiliwa Yanga, basi ni lazima awe anacheza katika kikosi cha kwanza katika timu, tunataka kuwa na timu bora kwa maana mchezaji atakayekuwa anakaa benchi, basi kiwango chake kifanane na yule atakayekuwa uwanjani anacheza.
“Tunataka kuona ushindani wa namba katika timu na tayari tumefanikiwa kumalizana na wachezaji wawili ambao mikataba yao imemalizika ambao ni Morrison na Tshishimbi,” alisema Hersi.GSM chini ya uongozi wa Yanga umepanga kufanya usajili wa kisasa na kati ya wachezaji wanaotajwa kutua ni Salum Abubakary ‘Sure Boy’ kutokea Azam, Heritier Makambo (Horoya AC), Jimmy Ukonde (UD Songo) na Tuisila Kisinda (AS Vita).
KIUNGO MKENYA AKUBALI KUTUA YANGA
Katika hatua nyingine, baada ya kuenea kwa tetesi za kiungo wa Kariobang Sharks ya Kenya, Yidah Sven kutakiwa na Yanga, mwenye amekubali msimu ujao kuvaa jezi ya klabu hiyo.
Rafi ki wa karibu wa kiungo huyo raia wa Kenya, ameliambia Spoti Xtra kuwa: “Yidah anaipenda sana Ligi ya Tanzania, amevutiwa sana na Yanga kutokana na ukubwa wa timu hiyo, hivyo kama Yanga watakuwa tayari kumsajili yupo tayari kabisa.
”Alipotafutwa Yidah ili azungumzie ishu yake ya kutua Yanga, alisema kuwa kazi yake ni kucheza mpira, hivyo yupo tayari kucheza Yanga kwani amekuwa akivutiwa na wachezaji kama Papy Tshishimbi na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
“Kazi yangu ni kucheza mpira, hivyo nipo tayari kucheza Yanga kama itanihitaji kwa kuwa ni timu kubwa na yenye wachezaji wazuri kama Feisal Toto na Tshishimbi ambao natamani kucheza nao,” alisema kiungo huyo.

