WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu leo Aprili 24, 2020 amesema wagonjwa 37 wa Corona nchini wamepona na hivyo kufanya jumla ya watu waliopona ugonjwa huo mpaka sasa kufikia 48.
Waziri Ummy aliyasema hayo wakati akipokea msaada wa sabuni na fedha Sh. Milioni 50 kutoka Kampuni ya Azania Group kwa ajili ya mapambano ya Corona.
Alisema, wagonjwa hao 37 ni kati ya wagonjwa 108 ambao vipimo vya awali vimeonesha hawana ugonjwa wowote hivyo kusubiri vipimo vya mwisho ili waweze kuruhusiwa.
“Watu hawa 108 kama alivyosema mheshimiwa rais hawana dalili zozote za ugonjwa kama vile homa au mwili kuchoka isipokuwa wapo katika vituo vya matibabu kusubiri vipimo vya mwisho ili kuthibitika kwamba hawana virusi vya Corona kabla ya kuruhusiwa kutoka vituoni,” alisema Waziri Ummy na kuongeza.
“Hivyo leo nitoe habari njema, tumeruhusu watu 37 wameenda nyumbani na vipimo vyao vimeonesha hawana maambukizi ya Covid-19, kwa hiyo nitoe wito kwa jamii tusiwanyanyapae. Ni wenzetu tusiwanyanyapae,” alisema Ummy.
Waziri Ummy alisema, anaamini nchi itaishinda vita vya Corona.
“Binafsi nikiwa waziri wa afya ninaamini kabisa tutaishinda Corona Tanzania. Tutaishinda Corona bila kupata madhara makubwa kama waliyopata katika nchi nyingine,” alisema Ummy.
Waziri Ummy alisema, tangu Machi 16, mwaka huu nchi ianze kupata maambukizi ya ugonjwa huo hatari unaoisumbua dunia, kumekuwa na jumla ya maambukizi ya watu 284 ambapo kati yao, 10 walifariki dunia kutokana na ugonjwa huo na kubaki na idadi ya wagonjwa 274.
Kati ya hao wagonjwa 274, wagonjwa 11 walisharipotiwa kupona na nchi ikabakiwa na wagonjwa 263.
Katika wagonjwa hao 263, 108 ndio ambao vipimo vya awali vinaonesha hawana maambukizi huku 37 kati yao wakiruhusiwa.
Hivyo kwa sasa nchi ina wagonjwa 226.
STORI NA RICHARD BUKOS | GPL


