NAIBU Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara amesema kwa mujibu wa Barua iliyodaiwa kuwa ni ya Chadema iliyoandikwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na kueleza kuwa chama hicho kimemfuta uanachama Boniface Jacob, tayari amepoteza sifa za kuwa Diwani na Meya.
Akizungumza na Global TV Online nje ya Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, Waitara amesema; “Nimeiona barua ya Chadema, nimeona barua aliyowajibu Mkurugenzi wa Manispaa, nimesikia saiti ya Mnyika akizungumzia suala hilo.
“Niseme tu kwamba si kazi ya Mkurugenzi kusoma na kuelewa katiba ya Chadema inasemaje, ameshapokea barua ya Chadema na akawajibu kwa maandishi kuridhia maamuzi yao, ameshamaliza kazi yake, wala wasitegemee ataandika batua ya kukanusha, hivyo Jacob si meya tena wa Ubungo….
“Kama anaona haikuwa halali aandike barua kwa waziri mwenye dhamana kuomba marejeo, waziri atapitia na kutoa majibu au aende mahakamani,” amesema Waitara.
Hivi karibuni kuna barua ambayo ilisambaa mitandaoni ikidaiwa kuandikwa na uongozi wa Chadema Wilaya ya Ubungo kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ikieleza adhima ya kumvua uanachama wa Chama hicho, Diwani na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kwa madai ya kutumia makundi ya vijana kuchonganisha na kukigawa chama, lakini uongozi huo ulikana kuandika barua hiyo.
Hata hivyo barua nyingine ilisambaa pia ikidaiwa kuandikwa na Mkurugenzi wa Ubungo ikikiri kupokea taarifa ya Chadema kumvua uanachama Jacob hivyo kupoteza sifa za kuwa Meya wa Ubungo.
