JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wa ujambazi akiwemo mganga wa kienyeji wakiwa na silaha mbili za moto kwa ajili ya kufanyia matukio ya kiuhalifu mkoani hapa.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani hapa, kamanda wa polisi Jonathan Shana amesema jeshi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa ambao ni Steven Godfrey (32) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Yunusi Hamed (37) mkazi wa jijini Tanga, Said Hamisi (38) mkazi wa jijini Dar es Salaam na Msafiri Yohana (22), mkazi wa Jiji la Mwanza.
“Mnamo tarehe 6 mwezi wa tano, mwaka huu majira ya saa nne usiku maeneo ya daraja la Nduruma, Kata ya Baraa Halmashauri ya Jiji la Arusha, jeshi letu lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wa ujambazi waliokutwa na bunduki moja na bastola moja zenye jumla ya risasi 12,” alisema kamanda huyo na kuongeza.
“Majira ya saa nne baada ya kupata taarifa za kiitelejensia, tuliweka mtego maeneo ya Daraja la Mto Turuma ndipo tulipowaona watuhumiwa hao waliotokea Dar es Salaam kuja Arusha kwa kutumia gari aina ya Toyota Crown, lenye namba la usajiri T 777 DSJ ndipo tulipolisimamisha gari hilo lakini walikaidi amri.
“Hata hivyo, askari walichukua uamuzi wa kufyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatahadharisha lakini waliendelea kukaidi amri hiyo ndipo askari walipoamua kufyatua risasi kwa kulenga matairi ya gari hilo hali iliyosababisha kufanikisha ukamataji wa watuhumiwa hao huku mmoja wao aitwaye Msafiri Yohana akiwa amejeruhiwa kwa risasi katika viganja vyake vya mikono,” alisema Kamanda Shana.
Aidha, kwa mujibu wa Kamanda Shana, katika upekuzi wa gari hilo kulikutwa na aina za silaha mbili Shortgun (1) na bastola 1 zenye risasi nne za bunduki aina ya Shortgun na risasi nane za bastola zilizokuwa kwenye magazine pamoja na mikasi mitatu ya kukatia vyuma, nondo mbili, gundi na madawa mbalimbali ya mitishamba.
Alilisema, katika mahojiano na jeshi la polisi, watuhumiwa hao wamekiri kuja Arusha kwa lengo la kufanya uhalifu na watafikishwa mahakani pindi upelelezi utakapokamilika ambapo akatoa wito kwa watu wote wenye nia ya kufanya uhalifu kuwa watafanikiwa kuingia lakini watatoka majivu.
“Pia niwaombe wananchi waendelee kutoa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu kwa jeshi hilo ili waweze kuzifanyia kazi hali itakayosaidia kuimarisha utulivu, amani na usalama tulivu uliyopo,” alisema Kamanda Shana.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alilipongeza jeshi hilo kwa kufanya kazi zake kwa weledi na kuwataka wananchi kufuata maelekezo ya kutii sheria bila shuruti na wanaoshindwa wamekuwa wakishurutishwa kama hao.
“Kila wakati jeshi limekuwa likiwataka wananchi kutii sheria bila shuruti na wanaokaidi mmekuwa mkiwashurutisha. “Leo mmeonyesha mfano mmekamata majambazi wametii sheria na hawakuuawa na matokeo yake ni tofauti na huko nyuma wengi walikuwa wakikaidi na kujikuta wakiuwawa,” alisema Gambo. Na Ahmed Mahmoud, Arusha!
Na Ahmed Mahmoud, Arusha!





