
WAKAZI wa Njiapanda ya Mbezi Makabe Kuelekea Mpiji Magohe Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam,wameiomba serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) kufanya matengenezo ya barabara yake ili ziweze kupitika kirahisi na kuondoa usumbufu ambao anachangia magari kuharibika haraka.
Wakazi wa maeneo hayo wakizungumza na Global Publishers wamesema kuwa barabara hiyo ni mbovu na baadhi ya watu wanalazimika kulipia gharama ya kupaki magari yao kwenye vituo vya mafuta kwa kuwa wanashindwa kufika nayo majumbani kwao.
Salome Samuel mkazi wa mtaa wa Auleke alisema, katika kipindi hiki ambacho mvua bado zinaendelea kunyesha kwa wingi, hali inakuwa mbaya zaidi na kukwamisha shughuli zao.
Alisema, katika barabara hiyo kuanzia Njiapanda ya kuelekea Makabe imeharibika mno na hivyo kuiomba serikali kunusuru adha hiyo ambayo imepelekea mifereji kuziba kutokana na kujaa mchanga na takataka mbalimbali.