×

Kabudi: Dawa ya Madagascar Inafanyiwa Utafiti Kwanza – Video

WAZIRI  wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Profesa Palamagamba  Kabudi, amesema  yeye na wenzake waliokwenda Madagascar  kuchukua dawa ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona yanayosababisha ugonjwa wa Covid-19, hawajaja na dawa hiyo kwa ajili ya kuwagawia Watanzania bali wataifanyia kwanza utafiti na uchambuzi na wakiridhika nayo ndipo itaanza kutolewa kwa wananchi.

 

Kabudi ameyasema hayo leo Mei 9. 2020 jijini  Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kurejea nchini usiku jana Ijumaa kutoka Madagascar  ambako alikwenda  na wataalam wa masuala ya tiba  kwa maelekezo ya Rais John Magufuli aliyewasiliana na Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina.

 

“Tumerudi kutoka Madagascar jana usiku ila hatujaja na dawa ya kuanza kugawa leo, tumekuja na dawa za kuanza utafiti na uchambuzi wa kimaabara.  Nimepokea simu nyingi na  meseji za WhatsApp, watu wanataka niwagawie.  Jamani sina dawa, sijaja na chupa za dawa,” alisema Kabudi.

 

Alifafanua kwamba Madagascar wameijaribu wakajiridhisha kwamba ni salama ndiyo maana wanaitumia lakini akasema  lazima waifanyie kanza utafiti na wajiridhishe kuwa inafaa na kwamba wako tayari kuchukua mzigo wowote na popote pale itakapopatikana.

 

Alisema wamepewa chupa mbili tu ambazo zitasaidia pale wataalamu watakapochanganya dawa na kufanya utafiti na uchambuzi ili waone kama wamepatia.

 

“Tumepewa  chupa tatu za dawa itakayotumika kama tiba na maboksi manane ya  dawa itakayotumika kama kinga.

 

“Hatukwenda kuchukua ‘Kikombe cha Babu’,  ile ni dawa ya kisayansi, ndiyo maana tumeenda na wataalamu, mimi peke yangu kwa kuwa ni waziri nimepata bahati ya kugonga ile dawa, ila zile chupa tumekuja nazo mbili tu za kusaidia utafiti, hatuna dawa kugawa,” alisema akiwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari hata kama kuna dalili za uwepo wa matumaini ya dawa.

Leave a Comment