×

Rais Samia: Serikali Haitatoa Ruzuku kwa Sekta ya Madini, Amani Ni Msingi wa Dira 2050 – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali haitatoa ruzuku kwa sekta ya madini kwa sasa, akieleza kuwa wadau wa sekta hiyo wana uwezo wa kujiendesha wenyewe bila kuhitaji msaada wa kifedha kutoka serikalini.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Agosti 3, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi wa nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mkutano wa Mazungumzo Maalum kati ya Serikali na Sekta Binafsi.

Akizungumza na wadau wa sekta ya madini, Rais Samia alisema baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wana uwezo mkubwa wa kifedha, kiasi cha kugharamia shughuli za kifahari kama harusi zinazotumia helikopta, hivyo hakuna sababu ya Serikali kurejesha fedha za walipa kodi kwa njia ya ruzuku.

“Sekta hii ina uwezo mkubwa wa kujiendesha. Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji badala ya kutoa ruzuku,” alisema.

Badala ya ruzuku, Rais Samia alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu na mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa sekta ya madini. Miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa ni ujenzi wa Soko la Kimataifa la Madini, ambalo linatarajiwa kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini na kupanua fursa za biashara katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu nchini, akieleza kuwa ndiyo msingi wa mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Niendelee kusisitiza kuwa amani na utulivu ni mtaji mkubwa kuliko mitaji mingine yote. Kama hakuna amani na utulivu, Dira ya Taifa 2050 haitatekelezeka na hatutaweza kufanya chochote. Niwaombe Watanzania wote, sekta ya umma na sekta binafsi, tuweke amani mbele. Lolote unalohisi litavunja amani, usiliunge mkono,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewataka Watanzania kushirikiana kulinda amani, akieleza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo yatakayowezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo, kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi wa taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Comment