MABOSI wa Yanga mkononi wana majina zaidi ya matano ya washambuliaji ambao wanawahitaji kwa msimu ujao kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.
Miongoni mwa majina hayo ambayo mabosi wa Yanga wanayajadili kwa ajili ya kuwasajili ni Mghana, Michael Sarpong na Mkongomani, Heritier Makambo.
Kwa mujibu wa uchunguzi ambao umefanywa na Championi Jumatano, umebaini kwamba mashabiki wengi wa kikosi hicho wanamuhitaji zaidi kumuona Makambo aliyeenda Horoya AC mwanzoni mwa msimu huu akirejea kikosini hapo kuliko Sarpong aliyeachwa na Rayon Sports ya Rwanda.
Uchunguzi huo umebainisha Wanayanga wanamuhitaji Makambo kwa kile ambacho alikifanya kwenye klabu hiyo msimu wa 2018/19, ambapo alifunga mabao 17 na kuwa kinara wa ufungaji kwenye timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.Lakini pia suala lingine ni tayari Mkongomani huyo ameshaijua vizuri Ligi Kuu Bara baada ya kucheza msimu uliopita hivyo hata akirejea hatapata shida kucheza kwenye viwanja vya mikoani tofauti na Sarpong ambaye atahitaji muda zaidi.
Uchunguzi huo ulienda mbali kwa kuona pia Makambo tayari ameshazoea mazingira ya klabu hiyo, kimfumo, kuzoeana na wachezaji wenzake hivyo atafiti kwa muda mfupi katika kikosi cha kwanza tofauti na Sarpong ambaye atahitaji muda mrefu kuweza kuzoeana na wenzake.
Lakini kitu kimoja ambacho kinaonekana kuwa kigumu kwa Makambo kurejea haraka Yanga ni kutokana na kufungwa na mkataba wa miaka miwili zaidi ambayo anayo Horoya ya Guinea tofauti na Sarpong ambaye ni rahisi kumpata kwani kwa sasa hana timu baada ya mkataba wake kuvunjwa na Rayon.
Katika Ukurasa wa Kijamii wa Instagram wa mashabiki wa Yanga unaofahamika kama Yanga Sc Group of Supporters wenye wafuasi zaidi ya laki mbili, waliweka picha ya Makambo na Sarpong ambapo walihoji nani zaidi kati ya wachezaji hao ambapo Makambo alionekana kumpoteza vibaya mwenzake kwenye komenti 108 zilizokuwa zimeandikwa hadi jana mchana.
Stori: Said ally, Dar es Salaam

