JESHI la Polisi linawashikilia watu wanne, watatu wa familia moja kwa tuhuma za kumuua kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni baba yao Lumba Nhalima (57), kisha kumkata sehemu zake za siri.
Tukio hilo limetokea Mei 10, Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi, Benjamin Kuzaga, amesema siku ya tukio watuhumiwa walimnywesha pombe nyingi baba yao ili ashindwe kujitambua.
Watuhumiwa Sali Lumba (32), Jonas Lumba (28), Paulo Lumba (19) na mtu mwingine ambaye alikuwa anakunywa naye pombe Thomas Malongo (54) walimfanyia Lumba kitendo hicho akiwa njiani kurudi nyumbani.
Kuzaga amesema baada ya uchunguzi walibaini kabla ya kifo chake marehemu alikuwa akilalamika kuwa watoto wake wakubwa wanne ambao ni wa mke mkubwa wanataka kumuua ili warithi mali zake.
Ameongeza kuwa watuhumiwa wamekiri kuhusika kupanga njama na kufanikisha mauaji hayo na jeshi hilo limetoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kuachana na dhana potofu za kujipatia kipato kwa njia ambazo si halali, ikiwamo imani za kishirikina.
