×

Mbunge Wa Wanawake Dar, Alivyozusha Shangwe Kwa Kinamama Lishe, Amuunga Mkono Rais Samia

Mbunge wa Viti Maalum Wanawake jijini Dar es Salaam, Janeth Mahawanga akizungumza kwenye mkutano huo.

Dar es Salaam 7 Machi 2024: Mbunge wa Viti Maalum Wanawake jijini Dar es Salaam, Janeth Mahawanga katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo amezua shangwe kwa kinamama wa Wajasiriamali wa Mama Lishe wa Jukwaa la Wanawake wa Kata ya Mbezi Juu, baada ya kuwapatia bure majiko ya gesi ili waachane na matumizi ya nishati chafu ya mkaa na kuni ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mbunge Mahawanga akizungumza baada ya kugawa majiko hayo aliwaambia kama kuna kinamama wengine wanaohitaji majiko hayo wajiorodheshe ili awamu inayofuatia kinamama lishe wote wanatakiwa nao kupata.

Mbunge wa Viti Maalum Wanawake jijini Dar es Salaam, Janeth Mahawanga (wa pili kushoto) akigawa majiko ya gesi kwa kinamama lishe.

Mbunge Mahawanga aliwaambia kinamama hao kuwa maendeleo makubwa wanayoyaona hivi sasa hapa nchini ambayo hayajawahi kutokea yamesababishwa na utawala bora wa Rais Mwanamke mwenzao Dk. Samia Suluhu Hassan hivyo wanachotakiwa ni kumuunga mkono kwa kumchagua kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani ili maendeleo haya yazidi maradufu.

Mbunge Mahawanga aliwaambia kinamama hao waangalie jinsi shule za kata zinavyodi kujengwa kila kona, Hospitali na Zahanati zenye huduma bora na madaraja kila kona hali iliyosababisha hivi sasa hata wajawazito wasihangaike kwenda mbali  kutafuta hospitali za kujifungulia kama ilivyokuwa zamani. Aliendelea kusema;

Ilikuwa ni neema kwa Mama lishe wakijichulia majiko kila mmoja analotaka.

“Sasa hivi mama mjamzito hana haja ya kwenda mbali na anapoishi kutafuta hospitali ya kujifungulia sasa hivi ni hospitali kila kona hiyo ni hatua kubwa sana ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita.

“Ukiangalia shule za msingi na sekondari sasa hivi kila kona zikiwa zimesheheni walimu, maabara na kila kinachohitajika  na zinatoa elimu bora ambapo tunaona jinsi wanafunzi wanavyoibuka na ufaulu mzuri kwenye shule hizo.

Mbunge Mahawanga akizungumza na mwanamke mjasiriamali aliyefika na bidhaa zake kwenye mkutano huo.

“Kwakusema kweli Mama yetu Dk Samia apewe maua yake jamani, nawaomba wanawake wenzangu ili mambo haya yazidi kunoga zaidi ya hapa katika uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani tumchague Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kishindo ili tuendelee kuifurahia zaidi nchi yetu”.

Pamoja na kumchagua Mama yetu Dk. Samia nafasi za chini pia kuanzia ngazi ya Serikali za Mitaa ambapo uchaguzi wake unafanyika mwaka huu nazo tuwape wanawake katika nafasi Udiwani na Ubunge hapo mwakani nazo tuwachague wanawake kwa wingi kwakuwa wanawake ni mahiri kiutendaji”. Alimaliza kusema Mheshimiwa Mahawanga huku akishangiliwa na kinamama hao.

HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS /GPL

Leave a Comment