×

Polisi Watanda kwa Diamond

TAHARUKI nzito! Katika hali ya kushangaza, Polisi wamekutwa wametanda nyumbani kwa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na kusababisha sintofahamu, IJUMAA WIKIENDA limeshuhudia tukio mwanzo mwisho, karibu!

 

Baada ya kutonywa na vyanzo vyake, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilifika nyumbani kwa staa huyo, Mbezi-Beach Kwa Zena jijini Dar na kuwakuta Polisi hao wenye silaha wakiwa wamefika na pikipiki (tigo).

 

ISHU NI NINI?

Kabla ya kuzungumza na walinzi wa Diamond au Mondi, IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na majirani ambao waliainisha sababu ya Polisi hao kutanda nyumbani kwa Mondi.

“Ni ile ishu yake ya msaada ambayo aliitangaza kwenye vyombo vyake vya habari (Wasafi TV na Wasafi FM) kutoa msaada wa kodi za miezi mitatu kwa familia za watu 500, sasa kwake hapa imekuwa vurugu.

 

SIO NYUMBANI TU…

“Mbali na hapa, kule ofisini kwake pia ni balaa; watu wapo kama wote. Watu wanaamini wakifika hapa au kule ofisini kwake, ndiyo watawahishiwa mchakato wa pesa hizo,” alisema jirani wa Mondi aliyejitambulisha kwa jina la Abdul.

 

JIRANI MWINGINE…

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na jirani mwingine aliyeomba hifadhi ya jina, ambapo alisema Mondi amejitakia mwenyewe kwani angeweza kufanya kimya kimya mchakato huo na kuongeza kuwa, kutokana na wingi wa watu mpaka wezi na majambazi wanaweza kuwepo kiasi cha kuhatarisha usalama wake.

 

“Yaani Diamond hili kajitakia mwenyewe, angefanya kwa siri haya yote yasingemtokea, hapo kuna wezi na hata majambazi. Hapa sisi tunahofia ukiachana na wizi ukiangalia watu wamejazana kuanzia asubuhi mpaka jioni, wengine hawana hata barakoa wamesongamana getini na wanatoka maeneo tofauti tofauti, si watatuletea Corona jamani,” alisema jirani huyo na kuongeza;

 

“Hivi tunashukuru angalau sasa hawa Polisi wamekuja, tunaona kunaweza kuwa shwari na ikiwezekana sasa wawatawanye na kuwapa utaratibu mzuri wa kupata hiyo misaada aliyoitangaza.”

 

MLINZI AWATAWANYA

Baada ya wale Polisi wenye silaha kufika, mlinzi wa Mondi alipata nguvu na ikabidi awafuate wale waomba msaada na kuwaomba waende kisha warudi siku nyingine kwa ajili ya kupewa pesa hizo.

 

“Nimetumwa na bosi niwaambie kuwa muende, ila muendelee kusikiliza redio ili mjue lini anatoa msaada tena, pia amesema hapa kwake siyo sehemu sahihi ya kutolea msaada, hivyo hawezi kutoa hapa bali anatolea kule ofisi za media yake,” alisema mlinzi huyo.

 

WATII…

Watu hao walitii agizo hilo wakaanza kuondoka eneo hilo wakiwa angali hawajaridhika, lakini hawakuwa na namna baada ya Polisi wenye silaha walikuwa wameshaimarisha ulinzi wakiwa makini na kazi yao.

 

WAOMBA MSAADA WANENA

IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na baadhi ya watu ambao walifika kwa ajili ya kuomba msaada ambapo mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Ashura, alisema kuwa ana karibu wiki anahudhuria kwa Mondi bila kufanikiwa na anaambiwa yupo ndani ila hajawahi kumtia machoni.

 

“Yaani unavyoniona hapa leo nina wiki, lakini huwezi amini, sijawahi kumtia Diamond machoni kwangu na ninaambiwa yupo ndani halafu nilichokuja kusikia ni kwamba Diamond anagawa pesa kwa majina, kuna watu maalum anawapa. “Yaani ni bora asingetangaza angefanya kimyakimya, hebu waone watu walemavu wanakuja hapa tangu asubuhi hadi jioni hawapati kitu, kama siyo anajichumia dhambi ni nini,” alisema Ashura.

 

MONDI ABADILI GARI AKITOKA

Mwingine alisema kabla ya Polisi hao kufika mahali hapo, siku zilizopita, Mondi alikuwa akilazimika kubadili gari ndipo atoke ili watu wasimjue.

“Yaani ametutesa sana, alikuwa anatuchenga akitaka kutoka mpaka abadili gari ndiyo aweze kutoka,” alisema mama huyo ambaye hakutaka kujitambulisha.

 

MONDI ANASEMAJE?

IJUMAA WIKIENDA liligonga geti la msanii huyo ili kutaka kujua kwa upande wake anazungumziaje ishu hiyo ya watu kurundikana kwa wingi nje ya nyumba yake wakihitaji msaada na ukiangalia hiki ni kipindi cha Corona, lakini hata hivyo baada ya kugonga alitoka mlinzi na kusema bosi wake huyo hawezi kuzungumza kwa wakati huo kwani yupo ndani anajiandaa kutoka.

 

“Bosi hawezi kuzungumza kwa sasa, halafu yupo ndani anajaribu nguo za kwenda kushutia video, hivyo hamuwezi kuongea naye,” alisema mlinzi huyo bila kutaja jina.

Baada ya muda IJUMAA WIKIENDA lilimshuhudia Mondi akichomoka na msafara wake kwenda kushuti huku hali ikiwa shwari.

 

MAONI YA WIKIENDA

Anachokifanya Mondi kinaweza kuwa ni kizuri, lakini kutokana na ukubwa wa jina na usalama wake, anatakiwa jambo hilo kuliondoa mikononi mwake na badala yake, angeliweka chini ya uongozi wake ili maisha yake yabaki kuwa private- Mhariri.

STORI: MEMORISE RICHARD NA KHADIJA BAKARI, DAR

Leave a Comment