
WAKATI waumini wa Dini ya Kiislam wakisherehekea Sikukuu ya Idd El Fitr, furaha yao imezidi maradufu baada ya maambukizi ya Virusi vya Corona kuendelea kupungua nchini.
Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Dk John Pombe Magufuli kutangaza kupungua kwa maambukizi hayo na kuruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na kidato cha sita kuendelea na masomo.
Pia Rais Magufuli alifungua shughuli zote za kitalii huku Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda akichagiza kwa kutangaza siku ya jana kuwa ni ya kusherehekea kwa kila familia kucheza muziki, baa na hoteli pia kufunguliwa.
MAOMBI MAALUM
Aprili, mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza siku tatu maalum za maombi ya kutokomeza virusi hivyo nchini.
“Ndugu zangu Watanzania, kutokana na Ugonjwa wa Corona, nawaomba tutumie siku 3 kuanzia Ijumaa, Aprili 17 hadi 19 Aprili, kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kulinda nchi yetu na tumshukuru kwa kutuepusha na ugonjwa huu,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, kwa mara nyingine, Mei 17, mwaka huu alitangaza tena siku tatu za maombi maalum ya kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi baada ya maambukizi ya virusi hivyo kupungua nchini.
Rais Magufuli aliwaomba Watanzania kupitia viongozi wa dini kufanya ibada ya shukurani kuanzia Mei 21 hadi 23 mwaka huu kutokana na matendo makuu ambayo Mungu amelifanyia Taifa kwa kuliponya na Corona.
Hadi Mei 23, mwaka huu, Tanzania ilikuwa na wagonjwa 509 na vifo 21 kutokana na ugonjwa huo wa COVID-19.
Misikiti na makanisa mbalimbali jana ilizizima kwa maombi hayo ambayo sasa yameendelea kutoa mwanga kutokana na maambukizi ya virusi hivyo kupungua nchini.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Baraza la Waislam wa Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma alishukuru namna ambavyo viongozi wa dini wameshirikishwa tangu mwanzo katika mapambano dhidi ya COVID-19.
“Sisi tunashukuru sana nafasi ya viongozi wa dini imekuwa kubwa tangu mwanzo… Rais ameendelea kututia moyo sisi viongozi wa dini na wananchi kwamba tukimtegemea Mungu, mambo yanawezekana,” alisema.
Akirejelea hotuba za Rais Magufuli ambazo amekuwa akihimiza wananchi kumtanguliza Mungu katika vita hii, Mruma alisema Rais Magufuli ametoa ujumbe wa matumaini unaosaidia kupambana na ugonjwa bila hofu. Anakiri kwamba, kupitia kwa Rais Magufuli, ipo nguvu ya matumaini iliyopatikana kutokana na ibada na sala zinazoendelea kwenye nyumba za ibada.
“Ni jambo la kumshukuru sana Mungu kwamba Rais wetu amekuwa msomaji wa maandiko juu ya namna Mungu anavyotusaidia… Rais amewapa watu matumaini.”
Wakati Rais Magufuli alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi kusimama na kubainisha msimamo wake wa kumtanguliza Mungu katika suala zima la mapambano dhidi ya COVID-19 kwa kuelekeza maombi ya kitaifa, amefuatiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye hivi karibuni alikaririwa akiwaambia Wamarekani kwamba, pia wamwamini Mungu, wataweza kushinda vita hiyo.
STORI: MWANDISHI WETU, DAR