×

Bosi Amzalisha Denti, Atoweka!

 

MFANYABIASHARA aliyefahamika kwa jina la Hassani Katundu, ambaye ametajwa kama bosi kwenye miradi yake, anadaiwa kumpa mimba na kumzalisha mwanafunzi wa kidato cha tatu mwaka huu katika Shule ya Msingi Miburani iliyopo Temeke jijini Dar.

 

Akizungumza na mwandishi wetu, mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Christina (sio jina halisi) mkazi wa Buza Mji Mpya, alisema aliingia kwenye mtego wa bosi huyo baada ya kuanza kushawishiwa kwa ukarimu wake.

 

“Sipajui anapoishi, lakini alikuwa akija jirani na nyumbani kwetu na kufikia kwa ndugu zake.

 

“Aliponiona, alianza kuonesha uungwana mkubwa sana, ndipo siku moja aliponiona karibu na nyumbani, akaniambia tufuatane kwa kaka yake ambapo siyo mbali na hapa nyumbani, ni hapo mtaa wa pili tu.

 

“Tulipofika kwa huyo kaka yake, tulimkuta ambapo huyo jamaa alimwambia kaka yake, ‘samahani naomba utupishe kidogo nataka niongee na mgeni wangu’.

 

“Huyo kaka yake alitoka na kutuacha wawili chumbani hapo, ndipo bosi huyo alitumia ushawishi mkubwa na kwakuwa mwenzangu ni mkubwa, hivyo alinizidi maarifa na kujikuta tunaingia kwenye kitendo kilichonisababishia huu ujauzito,” alisema mwanafunzi huyo.

SIRI YAFICHUKA

Wahenga walisema “Pembe la ng’ombe halifichiki” Hivyo ndivyo ilivyokuwa, siku zilisonga ndipo mama mzazi wa mwanafunzi huyo aligundua kuwa mwanaye anaujauzito.

 

Baada ya kumbana maswali, mwanafunzi huyo alimtaja jamaa huyo ambapo mikakati ya kumuita ikaanza.

 

“Kwanza nilianza kumwambia kuwa nimepata ujauzito kufuatia tuliyofanya siku ile, ambapo alikubali ila alinipa onyo nisimtaje kwa kuwa mimi ni mwanafunzi na kunishawishi ikiwezekana nimsingizie mtu mwingine naye angeendelea kunitunza kwa siri.

 

“Hilo kwangu lilikuwa gumu kwa kuwa sikuwa na mtu mwingine zaidi yake. Hilo nilimshirikisha mama ambapo aliamua kumuita, lakini badala ya kuja, alianza kumzungusha,” alisema mwanafunzi huyo.

 

“Mama alipoona anazidi kuzungushwa, ndipo akaenda kupeleka shauri hilo ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Buza, Kitengo cha Ustawi wa Jamii ambapo walimuandikia barua ya wito lakini hata hivyo badala ya kuja, yeye aliwaagiza wazazi wake.

 

“Wakiwa ofisi hiyo, wazazi hao waliambiwa kuwa wito huo haukuwa wao, bali wa mtoto wao ambapo wazazi hao walisema jamaa huyo yuko nje ya nchi.

 

“Walipoambiwa wamfikishie taarifa ya kuhitajika kwenye ofisi hiyo, wazazi hao walisema kwa sasa hawezi kuja kwa kuwa nchi aliyopo mipaka imefungwa kwa ajili ya Corona.

“Hivyo nimeteseka na ujauzito huu nikisaidiwa na mama yangu ambaye tunaishi katika mazingira magumu, ambapo mpaka sasa nimejifungua na mwanangu ana siku nane sasa hatuna pesa ya kumnunulia mtoto nepi wala sabuni au lishe kwa ajili yangu na mwanangu.

“Najuta sana, nimeharibu ndoto zangu kwa kurubuniwa, naomba kama kuna wasamaria wema, wajitokeze kunisaidia kumalizia masomo yangu huku nikimlea mwanangu,” alisema mwanafunzi huyo na kusita kuongea na kuanza kulia.

 

MAMA HUYU HAPA

Baada ya kuzungumza na mwanafunzi huyo, mwandishi wetu alizungumza na mama wa mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Prisca Abilahi ambaye alikuwa na haya ya kusema:

“Huyu ni mwanangu wa kwanza ambaye baada ya kuanza masomo, alionesha bidii kubwa sana darasani na hata alipofika darasa la saba, alipata ufaulu mkubwa.

 

“Aliendelea hivyo mpaka kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha pili ambapo nao alipata ufaulu wa daraja la tatu. ‘divisheni three’. Na kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, lakini yaliyotokea ndiyo kama hivyo tena, ndoto za mwanangu kufika mbali kimasomo ndiyo zimekatishwa na huyo baba aliyemzalisha mwanangu, mbaya zaidi amemtelekeza,” alisema mama wa mwanafunzi huyo.

 

Mama huyo alipoulizwa sababu za kutolifikisha polisi suala hilo, alisema; “Mimi nilijua huyo mwanaume ni muungwana na nilitaka kwanza tuyazungumze nyumbani kifamilia, akanidharau na bado nikaendeleza uungwana wa kulipeleka ofisi ya kata kama shauri la maelewano, bado naendelea kudharauliwa kwa kuambiwa mwanaume hayupo na hawezi kupatikana kiurahisi.

“Mara naambiwa na hao wazazi wake kuwa hiyo mimba haikuwa ya mtoto wao,” alisema mama huyo.

Leave a Comment