
UGONJWA wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona umeanza kupungua mashambulizi yake nchini Ukraine na watu wameanza kuruhusiwa kutovaa barakoa, kutoka nje na kuendelea na shughuli zao za kijamii na kimaendeleo kama wanavyofanya hapa nyumbani Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Juni 8, 2020, na Dkt. Lufunyo Edson, ambaye ni Mtanzania aishiye nchini Ukraine wakati akizungumza na kipindi cha Front Page cha Global Radio moja kwa moja kutoka Ukraine.
“Hapa Ukraine watoto wa chekechea wamesharuhusiwa kurudi shule na wanaendelea na masomo kama kawaida, sekondari na vyuo bado lakini na wao wanaendelea na masomo online.
“Marekani ni taifa lililofanikiwa kuudanganya ulimwengu kuwa ni taifa bora zaidi duniani, lakini hakuna kitu kama hicho. Haki haipo, polisi wanaua hadi watu 1,000 kwa mwaka lakini huwezi kusikia kwenye vyombo vyao vya habari.
“Hakuna njia moja unayoweza kusema imetumika ikafanikisha kupambana na Corona, kila nchi ilikuwa na njia zake, wengine lockdowns wengine hawakuwa na lockdowns; zote ni njia sahihi, kikubwa zimesaidia kupambana na Corona na imeondoka.
“Huku Ukraine hatukuwahi kunawa mikono, tulikuwa tunatembea na sanitizer zetu basi, Tanzania mmevunja rekodi kunawa kila dakika, tunawapongeza sana. Kwa sasa huku hakuna mtu anayevaa barakoa kwenye maeneo ya wazi.” amesema Dr. Lufunyo Edson.