
DAR: Miezi kadhaa imepita tangu kusambaa kwa taarifa kuhusu staa wa Bongo Fleva anayeitumikia Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ akidaiwa kutaka kujitoa kwenye lebo hiyo.
JINSI MAMBO YALIVYOKUWA
Awali, zilianza kusambaa tetesi kuwa Rayvanny au Vanny Boy yupo mbioni kujitoa Wasafi kwa maana ya kwamba anahitaji kuanza kujitegemea kimuziki.
Ikasemekana kwamba, zoezi hilo limefeli kwa sababu kama atatakiwa kujitoa kwenye lebo hiyo, basi atatakiwa kulipa shilingi milioni 300.
“Jamani kuna nini tena maana Rayvanny kafuta picha zote kwenye akaunti yake, kaanza kuposti upya, inasemekana anataka kuondoka WCB ili aanze kujitegemea mwenyewe kimuziki, lakini unaambiwa imekuwa ngumu kwa upande wake kwa sababu ameambiwa ili aondoke, inatakiwa alipe shilingi milioni 300 ili kuvunja mkataba.
“Kwa hiyo, bado yupoyupo tu haelewi afanye nini, unaambiwa kafulia balaa hadi mama wa mtoto wake (Fahyma) anatoka na madanga mengine huko nje ili apate mkwanja wa kujihudumia, yaani ana hali mbaya,” uliandika moja ya kurasa maarufu za udaku kwenye Instagram.
Katika harakati za kumtafuta Rayvanny, Gazeti la IJUMAA lilikutana na Fahyma ambapo alipotakiwa kusema anachokijua juu ya ishu hiyo, alisema maneno hayo hayana ukweli.
“Jamani hizo taarifa mimi mwenyewe nimeziona, lakini hazina ukweli hata kidogo. Ni uongo mtupu,” alisema Fahyma na kuongeza;
“Kha! Jamani siyo kweli, halafu mimi siyo mzungumzaji wa hilo. Hebu mtafuteni yeye mwenyewe ndiye atawapa majibu kamili.”
Baada ya kumkosa Rayvanny hewani, Gazeti la IJUMAA lilimvutia waya mmoja wa mameneja wa Wasafi, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ambapo simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa, ndipo lilipomtafuta meneja mwingine, Said Fela ‘Mkubwa Fela’.
Kwa upande wake, Fela alisema hawezi kuzungumzia mambo hayo.
“Sijapata taarifa kuwa Rayvanny anataka kuondoka Wasafi…” Alisema Mkubwa Fela na kuongeza;
“Mwisho wa siku nahisi wanaosambaza hizo taarifa ni watu wachache tu wasiopenda mafanikio yake ambao pengine wameamua kutoa hizo taarifa za uongo ili kumharibia sifa yake.
“Mimi naomba tuendelee kumsapoti na kusapoti kazi zake ili zifike mbali tuachane na hayo mambo ya mtandaoni, muda mwingine huwa mtu anajisikia tu kumchafua mwenzake ili nafsi yake iwe na furaha,” alisema Fela ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kilungule wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Madai ya Rayvanny kuondoka Wasafi, yanakuja miezi kadhaa baada ya staa mwingine wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ aliyekuwa chini ya lebo hiyo kujitoa na kwenda kuanzisha yake ya Konde Gang Music Worldwide.
Stori: MEMORISE RICHARD, Ijumaa