
BAADA ya kupita takribani miezi miwili na nusu bila ya kuchezwa mechi ya Ligi Kuu Bara, hatimaye jana Jumamosi ligi hiyo iliendelea kwa kuchezwa mechi mbili. Moja Shinyanga na nyingine Tanga.Leo Jumapili moto wa ligi hiyo utaendelea tena kwa kuchezwa mechi zingine mbili ambazo zote zitapigwa jijini Dar.
Mapema tu saa 10:00 jioni, katika Uwanja wa Taifa, Simba watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting, kisha usiku saa 1:00, Azam vs Mbao.Kuelekea mchezo wa Simba vs Ruvu, Simba wametamba wakisema: “Tunaendelea tulipoishia, tutaelewana tu.” Kauli hiyo ya Simba inakuja kutokana na wao kuwa karibu katika kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara ambapo hivi sasa wana pointi 71.

Wanahitaji kushinda mechi tano mfululizo kati ya kumi ili kuwa mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo.Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema: “Nayaona kabisa makombe matano mfululizo tukiyachukua. Kama Yanga ikiwa bingwa, basi mimi nitaacha kazi ya kuwa msemaji wa Simba kwa sababu mimi ni msemaji wa mabingwa.”
Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji, baada ya kuwanoa vijana wake kwa takribani wiki mbili huku wakicheza mechi mbili za kirafiki na kushinda zote, anaamini njia ya wao kuelekea kuwa mabingwa ni nzuri.Sven alisema wataanza na Ruvu, kisha Mwadui, baada ya hapo picha ya wao kuelekea kwenye ubingwa itakuwa imejichora kabisa.

“Wachezaji wanaonyesha morali ya hali ya juu na kujitahidi kufuata maelekezo yangu huku kila mmoja akihitaji kupewa nafasi ya kuanza kikosini.
“Hali hiyo inanipa nafasi kubwa ya kupanga timu na kuamua kina nani waanze,” alimaliza.Leo Simba itashuka dimbani bila ya huduma ya kiungo wake wa muda mrefu, Jonas Mkude ambaye ni majeruhi na Sharaf Shiboub aliyekwama kwao Sudan.

Upande wa Ruvu Shooting, Ofisa Habari, Masau Bwire, alisema: “Tunataka kuwa kikwazo kwa Simba, wamesema wanahitaji mechi nne ili kutwaa ubingwa, watuondoe kwenye hizo timu nne wanazozitaja.
“Utapigwa mpira wa Barcelona mpaka wao washangae kwa nini wamekutana na sisi, ninajua wengi wanafikiri tutafungwa ila hilo halipo.”Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 23, 2019, Simba iliichapa Ruvu mabao 3-0 Uwanja wa Uhuru, Dar.
STORI: LUNYAMADZO MLYUKA NA SAID ALLY,DAR