×

Winga AS Vita Ataja Siku ya Kutua Yanga

UKIONA hivi karibuni jembe jipya linatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar, basi fahamu huyo ni winga wa AS Vita, Tuisila Kisinda raia wa DR Congo.

Winga huyo ameliambia Spoti Xtra kuwa: “Muda wowote kuanzia sasa nitatua Tanzania kukamilisha usajili wangu wa kujiunga na Yanga.

 

”Hivi karibuni, Yanga chini ya Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia, Hersi Said, alisema wapo katika mkakati mzito wa kusajili winga machachari kutoka katika ligi tano bora Afrika, jambo ambalo linatoa mwanga mzuri kwa Kisinda kuwa mali ya Yanga.

 

Akizungumza na Spoti Xtra moja kwa moja kutoka DR Congo, winga huyo amesema wapo kwenye hatua nzuri ya kumalizana na Yanga, anachosubiri ni kuja kutia saini na kuwa mchezaji halali wa timu hiyo.

 

“Nipo kwenye mazungumzo na Yanga kwa muda mrefu sana na katika mazungumzo ambayo tumeongea, bado hatujamalizana. Nilitakiwa nitue Dar siku nyingi huko nyuma, lakini kuna vitu havikukaa sawa.

 

Ikashindikana.“Kwa sasa nasubiri kutumiwa fedha ambazo tulikubaliana ili nije huko, na kama nitatumiwa wiki hii basi wiki ijayo nitatua Dar kwa ajili ya kumalizana na Yanga,” alisema winga huyo.

 

Alipoulizwa Hersi juu ya ujio wa nyota huyo, alisema: “Kwa sasa tupo kwenye mipango ya kuhakikisha timu inafanya vizuri katika michezo ya ligi kuu, masuala ya usajili tusiyazungumzie kwanza ila baadaye kila kitu kitakuwa wazi kwa sababu tunataka kutengeneza timu ya ushindani zaidi.”

 

Ikumbukwe kuwa, wadhamini wa Yanga, Kampuni ya GSM, imekuwa ikipambana kuhakikisha timu hiyo inasajili wachezaji wazuri wa kuibeba timu katika michuano mbalimbali.

STORI NA MARCO MZUMBE, DAR

Leave a Comment