×

Dyana Nyange: Nimerudi Kundini!

“NAJUA unanipenda nami nakupenda wewe…

Unajua nakupenda nangoja uanze wewe…

Moyo wangu wakupenda wewe pekee…

Nivute kwako, nitoe huu upweke…

Nivute kwako baby…

Nivute kwako nitoe huu upweke…’’

Haya ni mashairi ya miongoni mwa nyimbo bora za Bongo Fleva za wakati wote. Ni Wimbo wa Nivute Kwako wa mwanamuziki mwenye kipaji na sauti matata. Wimbo huu ulifanya, umefanya na utafanya poa sana tangu mwaka 2011.

Wimbo huu ni kutoka kwa mwanamuziki wa kike wa Bongo Fleva, Mwanaisha Nyange almaarufu Dayna Nyange.

Mafungu ni ngoma iliyomtambulisha rasmi kwa mashabiki akiwa na mwanamuziki Lawrence Malima ‘Marlow’.

Dayna aliendelea kupasua na mikwaju mikali kama Nivute Kwako, Fimbo ya Mapenzi, I Do, Nitulize, Saresare, Komela, Angejua na nyingine kibao.

Dayna kwa sasa anafanya poa na mkwaju wake mpya wa Homa ambao ameuachia hivi karibuni na unakimbiza kwenye mitandao mbalimbali ya muziki ikiwemo YouTube.

IJUMAA WIKIENDA limepiga stori kibao na Dayna na amefunguka mengi ikiwemo ukimya wake kwenye gemu;

IJUMAA WIKIENDA: Dayna ulifanya poa sana kwenye gemu, baadaye ukapotea, tatizo ni nini?

DAYNA: Ni kweli nimekuwa kimya kwa sababu nilikuwa ninasafiri sana, kuna vitu nilikuwa ninavifanya kwa kipindi hicho.

IJUMAA WIKIENDA: Nini siri ya safari zako?

DAYNA: Ni biashara zangu nyingine tu, pia nilikuwa narefreshi kidogo.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa sasa umeachia ngoma mpya ya Homa, je, mapokeo yakoje?

DAYNA: Mapokeo ya ngoma yangu mpya ni mazuri sana, namshukuru Mwenyezi Mungu.

IJUMAA WIKIENDA: Mipango yako iko vipi kwa sasa ili kubaki kwenye chati?

DAYNA: Mimi naamini nilikaa nje ya gemu kwa muda mrefu, sasa nimerudi na nimepokelewa vizuri. Kiti changu hakuna wa kukikalia.

IJUMAA WIKIENDA: Soko la muziki limekuwa na ushindani, unalizungumziaje hili?

DAYNA: Kwa sasa ujanja umekuwa mwingi, hata mashabiki wanaupokea huo ujanja, tofauti na zamani na kwa sasa ubunifu ni mwingi.

IJUMAA WIKIENDA: Una kitu gani cha tofauti na wasanii wenzako?

DAYNA: Dayna ni mtu mpole, mtulivu na nina hofu ya Mungu, najua wapi nimetoka na ninapokwenda.

IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi uliachia Kaswida, je, uliacha muziki wa kidunia kwa muda tu?

DAYNA: Nilifanya vile kwa sababu ilikuwa ni kipindi cha Mfungo wa Ramadhani. Pia ni ndoto yangu kubwa kwa sababu mimi ni binti niliyelelewa katika maadili ya Kiislam.

IJUMAA WIKIENDA: Je, kuna siku utaacha muziki wa kidunia na kuendelea na Kaswida?

DAYNA: Kama nilivyosema, ilikuwa ni ndoto yangu, hivyo nina mpango baadaye kuendelea kuimba, ila itakuwa katika mfumo wa kutoa mafunzo.

IJUMAA WIKIENDA: Je, una mpango wa kuachia album?

DAYNA: Soko la album si zuri, ila ninawaza kuachia Extended Playlist (EP).

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu kwenda kimataifa?

DAYNA: Nina kolabo nyingi za nje kama Nigeria na Kenya. Nina kazi nyingi ambazo nitaziachia.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kweli mapenzi ndiyo sumu inayowamaliza wasanii wa kike?

DAYNA: Hapana, japo mapenzi yana nguvu kubwa. Unajua hadi mtu anaamua kuzama kwenye mapenzi, kuna vitu vingine ambavyo vinachangia, hivyo ni changamoto tu ambayo ipo.

IJUMAA WIKIENDA: Je, kwa upande wako unazungumziaje ishu ya Vanessa Mdee kuacha muziki?

DAYNA: Nimesikia alichokisema na ana sababu zake, yeye najua nini anakitaka au maumivu aliyopitia. Pia tumuombee ili arudi kuwa sawa.

IJUMAA WIKIENDA: Ulishawahi kupitia msongo wa mawazo hadi ukatamani kuacha muziki?

DAYNA: Hakuna biashara isiyokuwa na changamoto bali tunazidiana, siwezi kusema naulaumu muziki. Napenda kuwaambia wasanii tujitahidi kuwa na plan b ili tusiathirike sana, kuridhika na kidogo unachokipata.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani kinachowakwamisha zaidi wasanii?

DAYNA: Naweza kusema ni uoga tu, tunatakiwa kujitengenezea mazingira tu.

IJUMAA WIKIENDA: Kumekuwa na kitu kinachowaandama wasanii wa kike kuombwa rushwa ya ngono, je, unaizungumziaje hii?

DAYNA: Siwezi kusema ni changamoto kubwa, maana mtoto wa kike kutongozwa ni kawaida. Unaweza usitongozwe na prodyuza, ukatongozwa na mtu mwingine wa kawaida. Ni maisha ambayo yapo, ila ni jinsi ya kujiweka kwa watu na kujiheshimu.

IJUMAA WIKIENDA: Unakumbana na changamoto gani kwenye muziki wako?

DAYNA: Changamoto ni zilezile tu, kwenye kutafuta pesa lazima kuna changamoto, ni kupambana tu.

IJUMAA WIKIENDA: Unajivunia nini kwenye muziki wako?

DAYNA: Vipo vitu kadhaa ambavyo ninamshukuru Mungu na muziki, naweza kumtunza binti yangu bila kumtegemea mtu.

IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni single mama, unapitia changamoto gani kwenye malezi?

DAYNA: Hakuna changamoto kama umeamua kulibeba mwenyewe suala la malezi. Kwangu mimi inanipa moyo kupambana na kuhakikisha mwanangu anapata kila kitu.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI

Leave a Comment