
Idadi ya wagonjwa wa virusi vya coroa nchini Kenya imeongezeka na kufikia 7,577 baada ya wagonjwa 389 wapya kuthibitishwa.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema siku ya Jumamosi kwamba kati ya wagonjwa hao watatu ndio sio raia wa Kenya.
Miaka ya wagonjwa waliothibitishwa ni kati ya mwaka mmoja hadi miaka 93.
Bwana Kagwe alisema katika taarifa yake kwamba kati ya wagonjwa hao wapya , 243 wanatoka Nairobi, 36 kutoka Kajiado, 27 kutoka Kiambu, 23 kutoka Mombasa, 17 kutoka Busia na 10 kutoka Machakos.
Kaunti nyengine mbazo zilirekodi wagonjwa wapya katika kipindi cha saa 24 ni Migori 4, Kitui 6, Makueni 3, Uasin Gishu 3, Nakuru 3, Kilifi 2, Garissa 1, na Narok 1.
Waziri huyo alitangaza kwamba watu 88 zaidi wamepona kutoka hospitali na kufanya idadi ya waliopona hadi kufikia sasa kuwa 2,236.
Wagonjwa wengine 5 hatahivyo walifariki na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 159.
”Kupitia takwimu hizi , ni ishara kwamba tumepoteza maisha mengi, hatuwezi kukubali kupoteza maisha zaidi. Hivyobasi sisi kama taifa ni sharti kuheshimu masharti ya kukabiliana na ugonjwa huu la sivyo ugonjwa huu unaweza kuathiri vifaa vyetu vya afya”, alisema Kagwe.
Madai hayo ya Kagwe yanajiri huku baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya vikiripoti kwamba vyumba vya wagonjwa mahututi nchini Kenya vinakaribia kujaa wagonja wa corona.