
WAZIRI Mkuu wa Ivory Coast, Amadou Coulibaly, amefariki dunia jana Jumatano, Julai 8, 2020, jijini Abidjan ikiwa ni muda mfupi baada ya kuugua wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri la nchi hiyo na alikuwa amerejea hivi karibuni kutoka nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu ya moyo kwa miezi miwili.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 aliyezaliwa Februari 10, 1959, alikuwa amechaguliwa kuwa mgombea wa chama tawala katika uchaguzi wa mwezi Oktoba,mwaka huu baada ya Alessane Ouattara kusema kuwa hatowania tena muhula wa tatu.
Rais Ouattara ametangaza maombolezo ya kitaifa ya msiba huo huku akieleza kwamba Coulibaly alianza kuhisi vibaya wakati wa kikao cha kila wiki cha baraza la mawaziri na akapelekwa hospitali ambapo alifariki baadaye na kuwa kifo chake kitasababisha hali ya sintofahamu kuhusu uchaguzi huo.
Coulibali alifanyiwa upandikizaji wa moyo mwaka 2012 na alikuwa alikwenda Ufaransa Mei 2, 2020, ili kuwekewa bomba katika mshipa wake wa damu. Alirejea nchini kwake Alhamisi iliopita na kusema: “Nimerudi kuchukua mahali pangu kando ya rais , ili kuendelea na jukumu la kujenga taifa letu.”
Taarifa moja katika gazeti la Le Monde siku ya Jumatatu ilimnukuu afisa mmoja wa kigeni ambaye yumo nchini humo kama mchunguzaji wa uchaguzi huo ilisema: “Iwapo Gon Coulibaly hajapona, Ouattara atakuwa hana chaguo bali kuwania kwa muhula mwingine kwa sababu hakuna mpango mwingine.”
Suala hili kufikia sasa limekuwa mwiko kwa sababu rais amesema yuko tayari kuondoka na kutaja ni nani chaguo la mtu atakayemrithi. Chaguo la Ouattara kutowania urais mwezi Machi lilishangaza taifa hilo.
Wafuasi wa Ouattara wanasema kwamba ameleta ukuaji wa kiuchumi, udhabiti na kuimarisha sura ya Ivory Coast katika ngazi ya kimataifa lakini wanasiasa wa upinzani na raia wengi wa Ivory Coast wanasema kwamba rais huyo hakuwahudumia vya kutosha ili kuliunganisha taifa hilo na kuponya vidonda vya mgogoro mbaya ulioligawanya taifa hilo kabla ya yeye kuchukua madaraka.
Takriban watu 3,000 walidaiwa kufa katika vita vilivyosababishwa na mgombea Laurent Gbagbo aliyekataa kwamba ameshindwa uchaguzi wa 2010 na Ouattara, kabla ya vikosi vinavyomtii rais aliyekuwa madarakani kumkamata Gbagbo Aprili 2011.
Mgogoro wa kisiasa uliochukua muda mrefu kati ya Ouattara na rais wa zamani , Henri Konan Bedie, ulisababisha matatizo makubwa nchini Ivory Coast.