
BAADA ya kurejea kikosini, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison ameonekana kupewa mazoezi maalum ya kufunga huku ikielezwa ni kwa ajili ya kuiua Simba.
Morrison ambaye kwa siku za karibuni alikuwa na mgogoro na mabosi wake kiasi cha kutolewa kwenye timu, juzi aliungana na wenzake mkoani Kagera ambapo jana Jumatano walicheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, huku yeye akianza kikosi cha kwanza na kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0.
Mghana huyo ambaye alipeleka kilio katika mchezo uliopita walipokutana Yanga na Simba kwa bao lake la faulo ya moja kwa moja dakika ya 44 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara, kocha wake, Mbelgiji, Luc Eymael tayari amemuweka kwenye mipango yake.

Katika mipango hiyo, ameonekana kumpa mazoezi maalum ya kufunga kumuandaa na mchezo wa Jumapili hii dhidi ya Simba ukiwa ni wa nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar kuanzia saa 11:00 jioni.
Taarifa kutoka katika kambi ya Yanga iliyopigwa Kagera mapema wiki hii walipokuwa wakijiandaa kuwakabili Kagera Sugar, zinasema kujiunga kwa Morrison katika kikosi hicho imefufua matumaini mapya.
“Awali kocha Luc aliamua kumtoa Morrison katika mipango yake, lakini baada ya kuja katika mchezo huu dhidi ya Kagera, kocha ameonyesha kufurahishwa, hivyo ametumia mechi dhidi ya Kagera kumuangalia na kumuandaa ili aweze kuwa fiti kuwakabili Simba.
“Lakini kabla ya hapo, baada ya kutua tu kikosini alipokewa kwa shangwe kubwa ambapo kocha aliamua kumpatia mazoezi maalumu ya kufumania nyavu akiamini kwamba ile kazi aliyoifanya Machi 8, itajirudia,” alisema mtoa taarifa huyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema wanachokiangalia wao katika mchezo dhidi ya watani wao, Simba ni kuhakikisha wanafanikiwa kushinda na hawana wasi na hilo.
STORI: KHADIJA MNGWAI, DAR